Ulimwengu, Nyoni wafutiwa kadi nyekundu

WACHEZAJI wa Singida Fountain Gate, Thomas Ulimwengu na Erasto Nyoni wa Singida Fountain Gate wamefutiwa kadi nyekundu walizopewa katika mchezo uliozikutanisha timu hizo katika Ligi Kuu Bara ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ikielezwa kwamba zilitolewa kimakosa.
Ulimwengu na Nyoni walionyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo ambapo timu Singida iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kadi nyekundu zilitolewa tatu, huku mbili zikifutwa.
Katika mchezo huo wachezaji walioonyeshwa kadi ni Nyoni (Namungo), Dickson Ambundo (Singida Fountain Gate) na Ulimwengu.
Taarifa ya Bodi ya Ligi iliyotolewa leo imeeleza kuwa imefuta kadi za Ulimwengu na Nyoni baada ya kujiridhisha kupitia picha jongeo.
"Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imefuta kadi nyekundu walizoonyeshwa wachezaji Thomas Ulimwengu wa Singida Fountain Gate na Erasto Nyoni wa Namungo FC baada ya kujiridhisha kupitia Ushahidi wa picha jongeo na taarifa za wakufunzi wa waamuzi kuwa hawakustahili adhabu hiyo kwa kosa walilotenda," imesema taarifa hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Singida Fountain Gate, Hussein Masanza amesema: "Hii ni faida kwetu kuondolewa kwenye adhabu hiyo imetuongezea nguvu kumtumia mchezaji huyo ambaye ni muhimu kikosini."
Kabla ya kutua Singida Fountain Gate msimu huu, Ulimwengu aliwahi kuzichezea timu za Moro United, FC Väsby United, AFC Eskilstuna, Sloboda Tuzla, Al-Hilal na JS Saoura.
Kwa upande wa Nyoni aliichezea Simba kwa muda mrefu, huku Ambundo alicheza Dodoma Jiji na Yanga kabla ya kutua Singida Fountain Gate.