UJANJA TU: Pep anachambua matukio yote ya mechi nzima

Muktasari:

  • Atawafanyia tathmini timu pinzani, kila hatua ya mechi, kila tukio muhimu, ataendelea kuchambua namna mabao yalivyopatikana, hapo atagusia kwa uhakika bao lilipoanzia kutengenezwa hadi hatua ya mwisho ya mpira kuingia ndani ya nyavu.

KATIKA toleo lililopita kwenye uchambuzi wa kitabu cha Pep Confidential, mwandishi Marti Perarnau alielezea namna Kocha Pep Guardiola alivyo na tabia ya kuwafanyia tathmini wachezaji wake pamoja na kuyatambua matukio yote muhimu yaliyojitokeza katika mechi.

Sasa endelea…

Katika hii nusu saa inayovutia na ya kipekee, ambayo tumekaa kwenye kona ya mgahawa tukiguswa na hisia kama tuliochanganyikiwa kama vile ndio kwanza tuko katikati ya mechi inayoendelea, hapo Pep anakuwa mwenye kugusa matukio yote ya kuvutia yaliyotokea kwenye mechi.

Anaichambua mechi vipande vipande kama daktari anayetibu mgonjwa mwenye kuhitaji operesheni, ni kama anakuwa na fuvu alilolichambua mishipa yote, hapo anakuwa mwenye kumfanyia tathmini kila mchezaji wake, kila hatua ya mchezo na kila tukio muhimu.

Atawafanyia tathmini timu pinzani, kila hatua ya mechi, kila tukio muhimu, ataendelea kuchambua namna mabao yalivyopatikana, hapo atagusia kwa uhakika bao lilipoanzia kutengenezwa hadi hatua ya mwisho ya mpira kuingia ndani ya nyavu.

Baada ya hapo akili na fikra zake atazihamishia katika mechi nyingine, wakati akiendelea kupitia mechi nyingine kwenye video, ataanza kuzungumzia hiyo mechi nyingine itakavyokuwa, ataifundishaje timu yake katika wiki husika, nani atapumzishwa. Kitakachofuata baada ya hapo ni kutulia kidogo, kisha atakula mlo mdogo uliopo, wakati wote huo mvinyo ulioko pembeni ni kama vile haujaguswa, halafu atakubaliana na Torrent kabla ya mechi ijao watakachofanya ni mazoezi maalumu ya mipira ya adhabu.

Hapo hapo anaibuka Robben na wanakumbatiana, Robben wakati huo ameandamana na watoto wake wazuri watatu anamuaga, Pep naye anamkumbusha kasi aliyoionyesha na kuutumia mguu wa kulia dakika 10 kabla ya mechi kumalizika na kumhimiza afanye zaidi na zaidi.

Sekunde chache baadaye anajikuta akiipongeza kazi iliyofanywa na ocha wa Red Bull Salzburg, Roger Schmidt na kuanza kuchambua kwa mapana namna mabingwa hao wa Austria wanavyocheza, washambuliaji wao wanavyoshambulia, mabeki wa pembeni wanavyopanda na jinsi viungo washambuliaji wanavyotumia nafasi zao.

Wakati akitoa ufafanuzi na uchambuzi wa timu hiyo unaweza kudhani kwamba Salzburg ndio wapinzani wao katika mechi ya kesho ya Bayern, na hapo najikuta katika mshangao, ni kwa nini hasa ameamua kuzungumzia mambo hayo.

Hata hivyo huyo ndiye Pep, na dakika mbili baadaye anabadilika na kuanza kumzungumzia Iniesta jinsi anavyoipiga mipira yake kwa staili ya kuidokoa na kuwavuka mabeki wawili wa kati na jinsi ilivyokuwa na manufaa kwa Barca katika mechi yao na Espanyol jioni ile.

“Huo mchezo na tukio hilo uliangalia saa ngapi? Nilimuuliza, “si pale nilipokuwa nasubiri kwenye ule ukumbi, Iniesta ni wa aina yake, ni mtaalamu mwenye akili za kipekee.”

Huyo ndiye Pep katika kile anachokipenda na inafurahisha kuwa karibu naye, hii nusu saa ya kupata mvinyo na vitafunwa kidogo imekuwa kielelezo jinsi mapenzi yake katika soka yalivyo lakini pia ni somo la vitendo katika kuangalia mambo kwa mapana.

Siku moja usiku nilikuwa nimeandamana na Patricia Gonzalez, huyu ni kocha ambaye ni bado kijana, anainoa timu ya wasichana chini ya miaka 19 ya Azerbaijan. Tukiwa tunapata mlo wa jioni ghafla Pep akamgeukia na kumwambia, “Patricia naweza kukupa ushauri, , wakati wote chagua walio bora, wakati wote kuwa hivyo.”

Kocha huyu kijana hapo hapo akamuuliza swali zuri hasa. “Pep ni kina nani hao walio bora, je ni wale wachezaji ambao ni maarufu zaidi?

“Hapana, wachezaji wazuri walio bora ni wale ambao hawapotezi mipira, wale ambao wanajua kutoa pasi na ambao hawapotezi pasi wanazopewa, hao ndio walio bora, ni hao ambao ni lazima uwatumie kwa wakati wote hata kama wataonekana si maarufu kulinganisha na wenzao wengine kwenye timu.

Itaendelea Jumamosi ijayo…