Uchaguzi waipa Simba mamilioni

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Klabu ya Simba, Boniface Lihamwike (katikati).

KAMATI ya Uchaguzi ya Klabu ya Simba jana ilimalizia zoezi lake la awamu ya pili ya kufanya usaili kwa wagombea, huku watano wakifyekwa kabla hata ya usaili huo kwa kukosa vigezo vilivyotakiwa.

Wakati hao wakikatwa na majina ya waliopita kwenye usaili huo ambao ulifanywa kwa wagombea 23 yakitarajiwa kutangazwa leo, kamati hiyo imeiingiza klabu hiyo Sh 5.5 milioni zilizolipwa na wagombea wakichukua fomu. Wagombea wa nafasi ya mwenyekiti walikuwa watano na kila mmoja alilipa Sh 300,000 hivyo kuiingiza Simba Sh 1.5 milioni wakati kwa nafasi ya ujumbe kila mgombea mmoja alilipa Sh150,000 na jumla walikuwa 26, hivyo kuipa klabu Sh 3.9 milioni.

Hivyo, ukijumlisha fedha zote za wagombea 31 waliochukua fomu kwa nafasi wanazowania klabu imevuna jumla ya Sh 5.5 milioni, japo waliopitishwa walikuwa 23 tu kutokana na wengine kushindwa kukidhi vigezo. Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti Boniface Lihamwike juzi Alhamisi iliwafanyia usaili wagombea 11 ambao ni mchanganyiko wa nafasi ya mwenyekiti na wajumbe, hivyo jana walimalizia wengine 12.

Lihamwike alisema wanaendelea na zoezi hilo lakini leo majina ya wagombea waliopita yatabandikwa na hatua ya pingamizi itafuata.

“Kesho (leo) tutabandika majina hivyo nani amepita nani hajapita itajulikana siku hiyo,” alisema Lihamwike

Kwenye usaili wa kwanza wagombea nafasi ya Murtaza Mangungu na Geofrey Nyange ‘Kaburu’ walipangwa kufanyiwa siku moja.