Mambo mawili uchaguzi Simba

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Klabu ya Simba, Boniface Lihamwike (katikati).

ZOEZI la uchukuaji fomu za kugombea nafasi ya Mwenyekiti na Ujumbe wa klabu ya Simba lilifungwa rasmi juzi Jumatatu huku wagombea 29 wakirudisha fomu hizo na ili zipite kwenye mchakato huo basi kigezo cha maadili na masilahi ya klabu ndivyo vitazingatiwa zaidi.
Jana Jumanne, Kamati ya Uchaguzi chini ya Mwenyekiti Boniface Lihamwike walikuwa na kazi ya kukagua fomu zote za wagombea zoezi litalomalizika leo Jumatano na usaili utafanyika kuanzia Desemba 22 hadi 24 mwaka huu. Uchaguzi huo utafanyika Januari 29, mwakani.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Lihamwike alisema ukiachana na vigezo vyote vilivyopo kwenye Katiba ya Simba lakini vigezo hivyo pia vinajumuisha kwa maslahi ya Wanasimba wote.
“Unajua mgombea anaweza kuwa na sifa zote, vyeti vya shule, uzoefu katika soka hata zaidi ya miaka 10 lakini ikumbukwe kigezo cha Maadili na Maslahi ya klabu pia huzingatiwa kwa asilimia kubwa.
“Unapozungumzia masilahi ya klabu inapaswa kuangaliwa kwa mapana zaidi masilahi sio kutoa pesa tu kusaidia klabu ama namna nyingine yoyote bali hata kutosababisha mgogoro ndani ya klabu ambao utaleta mpasuko kwa wanachama. Hivyo hilo pia litaangaliwa,” alisema na kuongeza;
“Kwa mgombea yeyote ambaye hatapita kwenye hizi hatua zetu za awali atapewa nafasi ya kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kama ataona inafaa kufanya hivyo.”
Lihamwike alisema uchaguzi huu sasa unaonekana kuwa mgumu sana kwani wagombea waliochukua fomu ni wengi ukilinganisha na chaguzi zote alizowahi kusimamia za klabu hiyo ingawa ameahidi kuumaliza salama.
Aliwataja wagombea nafasi ya Mwenyekiti ni, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Murtaza Mangungu anayetetea kiti chake, Yusuph Omary Yenga.
Nafasi ya Ujumbe waliochukua fomu ni Abubakari Zebo, Abdallah Rashid Mgomba, Hawa Mwaifunga, Iddy Kajuna, Laurian Mganga, Elisony Edward Mweladzi, Lameck Lawrence, Nadir Atul, Omary Juma Mazora, Andala David Sizya, Christopher Kabalika Mwansasu, Hassan Bakar Kakayo, Isihak Ashraf Mukadamu, Seleman Haroub Said, Sharing Jumbe, Aziz Mohamed, Amina Ngaluma, Issa Masoud Idd, Hudhaifa R Kassim, Penda A Mapugilo, Injinia Rashid Khamis, Asha Baraka, Iddi H Kitete na Dr. Rehema A Simba.