TZ Prisons na utimamu wa mwili

New Content Item (1)
New Content Item (1)

WAKATI Tanzania Prisons ikiendelea kujifua kwa ajili ya mwendelezo wa Ligi Kuu, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ahmad Ally amesema kwa sasa anapambana utimamu wa mwili kwa nyota wake baada ya kurejea kambini.

Timu hiyo ilianza mazoezi mapema wiki iliyopita inajiandaa na mchezo ujao dhidi ya KMC, Aprili 12 mechi itakayopigwa Uwanja wa Sokoine, jijini hapa ukiwa wa raundi ya 22.

Wapinzani hao wanakutana ikiwa Prisons wapo nafasi ya tano kwa pointi 28 sawa na KMC, wakitofautiana mabao ya kufunga huku mechi ya mwisho zikitoshana nguvu kwa sare ya 1-1.

Ally alisema kwa sasa hajaanza kuelekeza mbinu za kiufundi badala yake ni kurejesha utimamu na kufungua mwili kutokana na wachezaji kukaa kwa muda bila mazoezi.

Alisema kwa siku takribani saba walizojifua, anaona yapo mafanikio kwa nyota wake namna wanavyorejesha ubora wake na kuanzia wiki hii wataanza rasmi masuala ya ufundi kwa ajili ya mechi zijazo.

“Kuna muda walienda mapumziko, yapo baadhi ya mambo lazima yapotee, kwa maana hiyo tunaanza kufungua miili kwa kuwajenga utimamu kisha wiki ijayo (hii) tunaanza mambo ya mbinu na ufundi,” alisema kocha huyo.

Kwa upande wake Nahodha wa timu hiyo, Benjamin Asukile alisema katika mechi tisa zilizobaki wanahitaji japo alama 12 ili kumaliza ligi wakiwa salama bila presha kama msimu uliopita.

“Malengo ni kushinda zote, ila kama itagoma basi mechi nne za nyumbani tushinde zote ili kufikia malengo ya nafasi nne za juu lakini tunahitaji kuondoa presha ya kukwepa kushuka daraja,” alisema mkongwe huyo.