Aziz Ki ampiga bao Guede Tuzo ya Ligi Kuu

Muktasari:

  • Aziz Ki ametwaa tuzo hiyo akiwashinda Kipre Junior wa Azam na Joseph Guede ambaye anacheza naye katika kikosi cha Yanga ambacho kinaongoza ligi.

KIUNGO Mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki ameteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Aprili wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2023/2024, huku kocha wake, Miguel Gamondi naye akibeba.

Aziz Ki ametwaa tuzo hiyo akiwashinda Kipre Junior wa Azam na Joseph Guede ambaye anacheza naye katika kikosi cha Yanga ambacho kinaongoza ligi.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), inaeleza kwamba: "Kwa mwezi Aprili, Ki alionesha kiwango kikubwa na kuwa msaada kwa timu yake katika ushindi wa michezo mitatu kati ya minne ambayo timu hiyo ilicheza, hivyo Yanga kukusanya alama 10 na kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi."

Yanga iliifunga Singida FG mabao 3-0, ikaifunga Simba mabao 2-1, ikaifunga Coastal Union bao 1-0 kisha ikatoka 0-0 na JKT Tanzania. Aziz Ki alicheza jumla ya dakika 359 za michezo hiyo.

Ndani ya michezo hiyo, Aziz Ki amefunga mabao mawili huku Guede akifunga manne jambo lililozua sintofahamu katika uchaguzi huo ukilinganisha na mchango wa mmoja baada ya mwingine.

Kwa upande wa Gamondi aliiongoza Yanga kukusanya alama 10 katika michezo minne waliyocheza, wakishinda mitatu na sare moja, hivyo kuendelea kuongoza ligi hiyo yenye timu 16.

Gamondi amewashinda Bruno Ferry wa Azam na Malale Hamsini wa JKT Tanzania alioingia nao fainali.

Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam, Amir Juma kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Aprili kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.

ORODHA YA WASHINDI TUZO ZA MWEZI

AGOSTI 2023
Kocha Bora: Miguel Gamondi - Yanga
Mchezaji Bora: Wazir Junior - KMC

SEPTEMBA 2023
Kocha Bora: Abdihamid Moallin - KMC
Mchezaji Bora: Wazir Junior - KMC

OKTOBA 2023
Kocha Bora: Roberto Oliveira - Simba
Mchezaji Bota: Aziz Ki - Yanga

NOVEMBA 2023
Kocha Bora: Bruno Ferry - Azam
Mchezaji Bora: Feisal Salum - Azam

DESEMBA 2023
Kocha Bora: Bruno Ferry - Azam
Mchezaji Bora: Kipre Jr - Azam

FEBRUARI 2024
Kocha Bora: Miguel Gamondi - Yanga
Mchezaji Bora: Leyi Matampi - Coastal Union

MACHI 2024
Kocha Bora: Bruno Ferry - Azam
Mchezaji Bora: Aziz Ki - Yanga

APRILI 2024
Kocha Bora: Miguel Gamondi - Yanga
Mchezaji Bora: Aziz Ki - Yanga