Twiga Stars kumaliza ukame WAFCON

Karata ya kwanza kwa timu ya taifa ya soka ya wanawake 'Twiga Stars' kusaka kufuzu Fainali ya Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) dhidi ya wenyeji wao Ivory Coast leo Septemba 22 katika Uwanja wa Yamoussoukro saa 12:30 jioni
Twiga Stars haijashiriki fainali za WAFCON kwa miaka 13 tangu ilipofanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 2010 zilipofanyika Afrika Kusini ambapo ilikuwa ni mara yake ya kwanza na ya mwisho kufanya hivyo na sasa inajaribu kusakaa nafasi ya ushirini kwa mara ya pili.
Ili ifuzu WAFCON, Twiga Stars italazimika kuitupa nje Ivory Coast katika raundi ya kwanza na ikifanikiwa hapo, itakutana na mshindi baina ya Djibouti na Togo katika raundi ya pili ambayo timu itakayoibuka mshindi itafuzu fainali hizo ambazo mwakani zitafanyika Morocco.
Twiga Stars iliposhiriki fainali hizo mwaka 2010 iliishia katika hatua ya makundi ambapo ilishika mkia kwenye kundi A baada ya kupoteza mechi zote tatu dhidi ya Nigeria, Afrika Kusini na Mali, ikifunga mabao matatu na kufungwa mabao nane.
Nigeria ndio mabingwa wa kihistoria wa WAFCON wakiwa wametwaa taji hilo mara 11 ambazo ni katika fainali za 1991, 1995, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2010, 2014, 2016 na 2018.