Tunaanzia hapa

Muktasari:

YANGA imeamua kuanza upya na leo mchana wataingia kambini eneo la Kigamboni chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mwambusi ambaye jana mchana alirejeshwa rasmi. Lakini kambi hiyo itakuwa na masharti mazito tofauti na ile ya Cedrick Kaze aliyetimuliwa. Sharti mojawapo ni mastaa wote lazima washinde kambini na hakuna kurudi uraiani mpaka msimu umalizike mwezi Juni na ambaye hataki yatamkuta makubwa kwa mujibu wa uongozi.

YANGA imeamua kuanza upya na leo mchana wataingia kambini eneo la Kigamboni chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mwambusi ambaye jana mchana alirejeshwa rasmi. Lakini kambi hiyo itakuwa na masharti mazito tofauti na ile ya Cedrick Kaze aliyetimuliwa. Sharti mojawapo ni mastaa wote lazima washinde kambini na hakuna kurudi uraiani mpaka msimu umalizike mwezi Juni na ambaye hataki yatamkuta makubwa kwa mujibu wa uongozi.


Habari zinasema Yanga wameamua hivyo baada ya kubaini Kaze alikuwa akiwapa bata sana mastaa hao kwa vipindi vifupivifupi baada ya mechi jambo wanalodhani lilichangia kuwatoa kwenye mstari tangu mzunguko wa pili uanze, ushikaji ulizidi.

BENCHI LA UFUNDI
Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla jana alimtangaza Mwambusi kurejea Yanga baada ya awali kuondoka kwa wiki kadhaa kwa maelezo kwamba alikuwa akijiuguza. Mwambusi ambaye ni Kocha wa zamani wa Mbeya City, Azam na Prisons anayesifika kwa mazoezi ya fiziki na nidhamu, alikuwa msaidizi wa Kaze kabla ya kujiweka pembeni kwa madai anakwenda kutibu jino. Lakini jana kwenye makao makuu ya Yanga, baadhi ya wanachama waliokuwa wamekaa vikundi walidai mbele ya waandishi haumwi aliamua kujiweka pembeni.

VIDEO: Mwambusi apewa mikoba Yanga


Mecky Maxime ambaye wiki moja iliyopita alitimuliwa Kagera, alikuwa akitajwa kwenye usaidizi Yanga hata kabla Kaze kuwasili ingawa dakika za mwisho aliwaringia na kubaki Kagera. Jana Yanga walikubaliana kuachana nae na kumrudia Mwambusi ambaye walikuwa na mkataba nae tangu uongozi wa Kaze. Straika wa zamani wa Yanga, Mkenya Ben Mwalala aliomba nafasi hiyo lakini wamempiga chini na hawakutaka kuangalia hata rekodi zake na Bandari ya Mtwara.
 
KOCHA MKUU
Kwa mujibu wa Msolla huyu atatajwa muda wowote na kwamba  ni Kocha mkubwa mwenye viwango vya kimataifa na mzoefu wa soka la Afrika. Lakini Mwanaspoti linajua kwamba Patrick Aussems maarufu kama Uchebe aliyewahi kutamba na Simba na sasa yupo AFC Leopards ya Kenya nafasi yake ni finyu. Uchebe aliliambia Mwanaspoti amesikia maneno mitandaoni lakini ni uzushi wala hajapigiwa.


Licha ya orodha ya makocha 50 walioomba, Yanga imeanza mazungumzo ya karibu sana na Kocha Mkuu wa Sudan, Mfaransa Hubert Velud ambaye pia hivi karibuni alishindwana na Simba dakika za mwisho.
Velud ana uzoefu na soka la Afrika na amekuwa akihusishwa na Simba tangu mwaka 2018 lakini wamekuwa wakiachana nae dakika za mwisho za makubaliano. Awali ilitokea hivyo wakamchukua Uchebe na wakati mwingine Sven Vandenbroeck. Velud amesaini mkataba mpya na Sudan mwezi Januari akichukua nafasi ya Zdravko Logarusic ambaye pia alishapita Simba akachemka wakampiga chini.
Kocha huyo mwenye miaka 60, amezinoa kwa nyakati tofauti Togo, JS Kabylie ya Algeria, TP Mazembe ya DR Congo na Etoile du Sahel ya Tunisia.
Velud aliinoa Togo ile ya kina Emanuel Adebayor mwaka 2009-2010, iliyokoswakoswa na mitutu ikielekea kwenye Afcon ya Angola.
Amewahi kuzinoa pia klabu ngumu za Kaskazini kama Hassania Agadir, ES Setif, USM Alger na CS Constantine zote za Algeria huku Sudan wakimtegemea kwa sasa awavushe kwenye kundi I lenye Morocco, Guinea na  Guinea-Bissau kuelekea Kombe la Dunia 2022, Qatar.
Kwa maoni kuhusu habari za ukurasa huu, tutumie: 0658-376417