Miezi 5 ya Kaze Yanga, sababu za kutimuliwa zafichuka

Dar es Salaam. Maisha ya ukocha ndani ya Yanga kwa Cedrik Kaze yamefikia mwisho juzi, baada ya miamba hiyo kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania.

Matokeo hayo yalikuwa miongoni mwa mwenendo mbivu wa kikosi hicho kwenye mzunguko wa pili, ambao alifanikiwa kushinda mchezo mmoja kati ya sita aliyoshuka uwanjani, akiwa na sare tano na kipigo mara moja.

Yanga, ambayo ilikuwa na matumaini ya ubingwa msimu huu baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza ikiwa juu kwa tofauti mbili, endapo Simba ingeshinda viporo vyake.

Lakini ilijikuta katika wakati mgumu baada ya kulazimishwa sare dhidi ya Mbeya City (1-1) Tanzania Prisons (1-1), Kagera Sugar (3-3), kisha kushinda dhidi ya Mtibwa (1-0), ikafungwa na Coastal Union (2-1) na juzi kulazimishwa sare ya 1-1 na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Mchezo huo, ulikuwa wa lazima kwa kaze kuibuka na ushindi ili kutuliza presha ya mashabiki na uongozi katika kurudisha pia imani ya ubingwa msimu huu.

Lakini licha ya kuongoza kipindi cha kwanza kwa bao safi la mshambuliaji wa Burundi, Fiston Abdulrazak, ilijikuta ikiruhusu bao hilo kurudi dakika moja kabla ya mchezo kumalizika, lililofungwa na nyota wao wa zamani, Pius Buswita.

Saa chache baada ya mchezo huo, Yanga ilitoa taarifa yake juu ya kuachana na benchi zima la ufundi lililokuwa chini ya kaze, hivyo kuwa na maana kwamba kocha msaidizi, Nizar Khalfan, kocha wa makipa, Vladmir Niyonkuru, kocha wa viungo, Edem Mortoisi na Ofosa Usalama, Mussa Mahundi.


Hatari ya Kaze

Kocha huyo mzaliwa wa Bujumbura alianza kuwa katika wakati mgumu baada ya kuanza kwa mzunguko wa pili.

Likizi ambayo wachezaji wake waliitumia haikuwa na matokeo mazuro tangu ilipoanza kufungwa kwa mara ya kwanza katika mchezo wa kirafiki dhidi ya African Sports ya Tanga.

Ilikuwa dalili mbaya ambayo kocha huyo bora wa Ligi Kuu kwa Desemba alishindwa kutambua mapema kitakachotokea.

Lakini baadaye, Sare ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine ilikuwa ni tukio jingine la kingele ya hatari kwa Kaze, ambayo hata hivyo bado haikusaidia kitu.

Kosa jingine dogo lilionekabna kuingia katika sababu za Kaze baada ya miamba hiyo kulazimishwa sare ya mabao 3-3 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Kwa mshangao wa wengi, Kaze aliamua kumpumzisha kiungo wake mpambanaji aliye katika kiwango bora, Mukoko Tonombe na kumpa nafasi Zawadi Mauya, aliyeonekana kuzidiwa katika eneo la katikati na kumbadilisha kumwingiza raia huyo wa DR Congo aliyemsawazishia bao la tatu.

Faraja ilirudi kwa ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar kwa ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkapa, lakini maswali yakaibuka baada ya kiungo wa Angola, Carlos Carlinhos kufunga bao pekee na kukataa kushangilia akionekana asiye na furaha.

Mchezo dhidi ya Costal Union ulikuwa msumari mwingine mgumu kuuvumilia kwa wanachama na mashabiki wa Yanga, achilia mbali uongozi wa Yanga wenye sapoti kubwa ya kampuni ya GSM.

Na hatimaye Polisi Tanzania wakahitimisha matatizo ya Kaze katika benchi la ufundi kwa kumrahisishia safari kwa sare ya bao 1-1 juzi jijini Arusha.

Hilo limekuwa gumu kwa uongozi kuendelea kulibeba baada ya kuona matumaini ya unigwa yameshaanza kukaa katika kona ya hatari zaidi.


Alipofeli Kaze

Licha ya matokeo yote ya mechi sita za mzunguko wa kwanza, Kaze alishindwa kabisa kuwa na mbinu mbadala ya kutafuta matokeo.

Hilo limefanya wadau wengi kudhani kuwa kocha huyo hakuwa na uzoefu wa kuendana na presha ya timu kubwa za Afrika kama Yanga.

Lakini kushindwa kupata safu nzuri ya kushambulia kwa muda wote ndani ya nyota 11 wa kwanza (first 11), lilikuwa tatizo jingine kwa kocha huyo.

Kaze mwenyewe

Katika salamu zake za kuwaaga wachezaji na mashabiki wa Yanga, kaze aliamua kuandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, jinsi ambavyo amefanya kazi kwa kipindi chote cha miezi mitano.

Alieleza pia namna anavyoondoka Yanga akiwa anaiacha ikiongoza kwenye msimamo wa ligi, lakini akabainisha kuwa katika kipindi alichokuwa Yanga alipata furaha pamoja na wakati mgumu pamoja.

“Ni mafanikio makubwa kwangu kufanya kazi na timu hii, namshukuru kila m,moja ndani ya klabu kwa kuniamini na kutimiza machache kati ya tuliyokubaliana,” aliseka Kaze.


Wadau wafunguka

Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi alisema Yanga inapaswa kujengwa zaidi uwanjani badala ya kutaka kushangiliwa tu na mashabiki inapofanya vizuri.

“Kaze si kocha mbaya na amefanya kwa kiwango kizuri na kwa wakati wake Yanga, lakini kwa Yanga timu ilipaswa kujengwa zaidi uwanjani na si kushangiliwa nje ya uwanja.

“Hata mbadala wa Kaze anahitaji kupewa taarifa za kutosha juu ya timu yake na awe na uhusiano wa kitaalamu zaidi na wachezaji,” alisema.

Madadi alitofautiana na beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Bakari Malima, ambaye aliunga mkono uamuzi wa klabu kuachana na Kaze.

“Tangu amejiunga na Yanga badala ya viwango vya wachezaji kupanda, ndiio kwanza vinaporomoka zaidi, jambo ambalo kwa mashabiki linawaumiza sana,” alisema Malima.

Hata hivyo, Malima pia amewashauri uongozi wa klabu hiyo, chini ya mwenyekiti, Mshindo Msolla kujitafakari ndani ya miaka miwili waliyokaa madarakani, nini wanajivunia?

“Msolla kitaaluma ni kocha, amenifundisha hata mimi timu ya Taifa 1997 hadi 2000, ajiulize shida ipo wapi, kama wanaomzunguka si washauri wazuri awaondoe ili asiendelee kuchafua CV.

“Pia kwanini hakuangalia uzoefu wa Kaze? Hawakujiuliza mara mbili wakati wanamsajili?” alihoji Malima.

Kocha na nyota wa zamani wa Pan African, Mohammed Adolph Rishard alisema kama uongozi ulimtimizia kila kitu na kocha akashindwa kufikia malengo, basi kufukuzwa haiwezi kuwa shida kwani ni jambo la kawaida kwa kocha yeyote duniani.

“Lakini kwa upande wa pili je wao wapo sawa?,” alihoji Adolf na kuendelea. “Hata kwa mrithi wa Kaze kuna mawili, akafanikiwa au kufeli, kwani atakapobadili mfumo ni dhahiri ataanza moja na kipindi hiki ligi inaelekea mwishoni,” alisema.

Aliyewahi kuwa mchezaji wa klabu za Simba na Yanga, Zamoyoni Mogela alisema kama Kaze alihusika katika usajili basi kutimuliwa ni sahihi.

“Unajua kama alihusika katika usajili kama ambavyo ilikuwa ikielezwa kutimuliwa ni sahihi, lakini kama alikuwa hausiki halafu amekuja kukutana tu na wachezaji ni tatizo kubwa kwani inawezekana wachezaji hawafiti katika mfumo wake,” alisema Mogella.

Mogela alisema Yanga wanahitaji utulivu sana katika kipindi hiki kwani mbio za ubingwa inaweza ikawa kwa kudra za Mungu.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Iddi Kipingu alisema haukuwa wakati sahihi kwa Yanga kuachana na kocha huyo.

“Hana rekodi mbovu ya namna hiyo hadi kuamua kuachana naye, walipaswa kumpa muda ili kuimarisha kikosi chake, tatizo kwenye soka letu tunataka timu itengenezwe hapo hapo na ichukue ubingwa hapo hapo,” alisema.

Ndoto ya Kaze kabla ya kutimuliwa ilikuwa kuipa ubingwa Yanga, aliamini katika hilo licha ya kupewa presha na Simba, kocha huyo Mrundi alisema nafasi ya ubingwa msimu huu iko wazi.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, kocha Kaze alisema mapngo wake ni kuipa Yanga ubingwa, japo timu yoyote kati ya Simba, Azam au hata Biashara zote zipo kwenye nafasi ya ubingwa pia, itategemea na namna walivyojipanga kwa mechi zilizosalia.