Tuna Saido, Fiston lazima tubebe ndoo

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Yacouba Songne amekiangalia kikosi cha timu yake hasa safu ya ushambuliaji kutokana na maigizo mapya ya Saido Ntibazonkiza na Fiston Abdul Razak na kusema kuna dalili zote chama lake msimu huu kubeba ubingwa.

Yocouba alisema muda wowote anatarajia kurejea tena uwanjani baada ya kuanza kupona vyema majeraha, lakini anachofurahi ni kuona eneo la mbele likiimarika kwa kuongezwa majembe ambayo anaamini yatauwasha moto kwenye duru la pili la Ligi Kuu.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Yacouba alisema hana wasiwasi na ubora wa kikosi chao kutokana na kukamilika karibu kila idara na kunusa harufu ya ubingwa, akisisitiza ni lazima wachezaji wapambane.
Raia huyo wa Burkina Faso alisema katika kuutaka ubingwa wa ligi ni lazima wajiandae kwa mechi ngumu zijazo za ligi ambazo wapinzani wana watajipanga kuwazuia, lakini amefurahi kuongezwa kwa kina Saido na Fiston ambao wakiungana na wao walioanza na timu, Yanga itatisha.
Mshambuliaji huyo alisema kutokupoteza mechi kutawafanya kukamiwa lakini pia kama wataendelea kushinda zipo timu zitataka kuwakwamisha katika mbio hizo.
“Tuna timu bora ambayo naiona imekamilika karibu kila idara, ukiangalia hata safu yetu ya ushambuliaji imeimarika zaidi na sasa imeongezewa watu zaidi, hii ni hatua njema kwa kuwa ushindani utaongezeka,” alisema Yacouba aliyefunga mabao manne mpaka sasa.
“Yanga kuwa bingwa inawezekana, lakini lazima kama timu tutambue hilo halitakuja kirahisi, tutahitajika kupambana na kuweka nguvu zaidi, zipo timu ambazo zitajiandaa kutukwamisha tusifikie malengo ugumu huo tukiweza kupambana nao na kuushinda ndio tutafanikiwa.
“Tunangoza ligi lakini pia hatujapoteza mechi sio kila mpinzani wetu anafurahia hilo na tutakavyozidi kukaa katika mazingira ya kuwa bingwa ndio ugumu zaidi utaongezeka, ni lazima tuwe jasiri zaidi katika mechi zetu.”
Kuhusu vita ya namba, Yacouba alisema kwa sasa na hasa baada ya usajili wa dirisha dogo, hakuna mchezaji mwenye uhakika wa namba.
Alisema usajili wao umeimarisha ushindani wa namba na sasa hata kama mchezaji akikosekana ni vigumu kuona pengo lake kutokana na kila mchezaji kuwa na ubora wa kuanza. “Ukiangalia kuanzia kipa mpaka huku mbele hakuna mchezaji ambaye ana uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza, kila mmoja ana ubora wa hata kuanza, hii inakufanya ukipata nafasi unatakiwa kuhakikisha unaonyesha vitu,” alisema.
Katika dirisha dogo mbali na Fiston, Yanga pia imemsajili beki wa kati Dickson Job na kuwapandisha vijana kutoka timu ya U20 na timu hiyo inatarajiwa kurejea kwenye ligi dhidi ya Mbeya City mchezo utakaopigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya.