Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mangungu kuanza na mambo 11 Simba

KLABU ya Simba jana ilipata Mwenyekiti wao mpya baada ya Murtaza Mangungu kushinda kwenye uchaguzi mdogo kwa kumbwaga Juma Nkamia na kuanika mambo 11 ambayo atayapa kipaumbele kwenye kipindi chake cha uongozi ndani ya klabu hiyo.

Mangungu alishinda kwa kishindo jana kwa kupata kura 802 kati ya 1140 zilizopigwa kwenye uchaguzi mdogo wa klabu uliofanyika jijini Dar es Salaam, ikiwa ni ushindi wa asilimia 70.35 dhidi ya kura 330 alizopata Nkamia ambazo ni sawa na asilimia 28.95.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Simba, Boniface Lihamwike ndiye aliyemtangaza Mangungu kuwa mwenyekiti mpya wa klabu hiyo akiziba nafasi iliyoachwa wazi na Swedy Nkwabi aliyejiuzulu ghafla Septemba mwaka juzi na nafasi yake kukaimiwa na Mwina Kaduguda tangu Novemba mwaka huo kabla ya kuitishwa uchaguzi huo uliomuingiza mwenyekiti huyo mpya.

“Waliopiga kura ni wanachama 1140, kura nane zimeharibika na Juma Nkamia amepata kura 330 sawa na asilimia 28.95,” alisema Lihamwike jana akitangaza matokeo ya uchaguzi huo.

Baada ya ushindi huo, Mangungu alizungumza na gazeti hili na kueleza kwamba katika uongozi wake atayapa kipaumbele mambo 11. Moja ya mambo hayo ni klabu kuwa na akademia na mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu.

“Siwezi kuyataja yote kwa wakati huu, lakini katika uongozi wangu na mambo 11 nitakayoyapa kipaumbele, ikuwamo ili la mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ambalo ni suala la kisheria.

“Ndani ya siku 69 tutakuwa tumefikia hatua nzuri kama sio kulikamilisha kabisa,” alisema Mangungu, Mbunge wa zamani wa Kilwa Kaskazini.

Aliongeza katika uongozi wake hatapenda kuona makundi ya watu waliokuwa wapambe wake au wa mpinzani wake Juma Nkamia.

“Simba ni nguvu moja, sitapenda kuona makundi ya uchaguzi yanaendelea, tuungane kwa pamoja tufanye kazi ili kuipa mafanikio klabu yetu kitaifa na kimataifa,” alisema.

Kwa upande wa Nkamia alimpongeza Mangungu kwa ushindi na kueleza kwamba pamoja na wajumbe ‘kumtosa’ ataendelea kuwa mwanachama ndani ya klabu hiyo.

“Nimuombe tu Mangungu kusimamia ipasavyo mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji, akifanya hivyo na mchakato ukakamilika hata mimi nitaingia kununua hisa,” alisema Nkamia.

Katika uchaguzi huo wa jana ulioanza mapema asubuhi na kukamilika saa 8 mchana, viongozi na wanachama maarufu wa Simba wakiwamo Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo walihudhuria isipokuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mohammed Dewji’ aliyeelezwa yupo safarini.

Aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda akihojiwa mapema alisema; “Mwenyekiti ninayemuachia nafasi hii namuachia Simba iliyonona. Mwenyekiti anayekuja mpeni ushirikiano tukawe klabu kubwa zaidi Afrika.”

Mwenyekiti huyo mpya wa Simba, amezaliwa September 29, 1959 na alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na kukaa kipindi kimoja tu kwani Uchaguzi wa mwaka 2015 aliangushwa na Vedastor Ngombare na ni mtu ambaye amekuwa mwanachama wa Simba anayejitolea kwa hali na mali kwa muda mrefu mpaka alipojitokeza kuwania nafasi hiyo akiwa miongoni mwa wagombea wawili waliopenya kwenye mchujo.