Tujifunze kwa Kagere, Victor Wanyama

Muktasari:
- Ni jambo lililotushtua kidogo hapa kijiweni kwa vile umri wa Kagere umesogea kwani mshambuliaji huyo ana umri wa miaka 38 hivi sasa na ana muda wa takribani miaka mitatu hajaichezea timu hiyo kwani mara ya mwisho kuitumikia ilikuwa ni 2022.
JANA kocha wa timu ya taifa Rwanda ‘Amavubi’, Adel Amrouche alitangaza kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki mwezi ujao dhidi ya Algeria mwezi ujao ambapo alimjumuisha nyota wa Namungo, Meddie Kagere.
Ni jambo lililotushtua kidogo hapa kijiweni kwa vile umri wa Kagere umesogea kwani mshambuliaji huyo ana umri wa miaka 38 hivi sasa na ana muda wa takribani miaka mitatu hajaichezea timu hiyo kwani mara ya mwisho kuitumikia ilikuwa ni 2022.
Na pia msimu huu Kagere hajaonyesha sana makali yake ya kufumania nyavu akiwa na kikosi cha Namungo, lakini Amrouche ameona amjumuishe katika kikosi chake.
Kwingineko kocha wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, Benni McCarthy amemjumuisha kiungo mkongwe Victor Wanyama katika kikosi chake ambacho kitacheza mechi ya kirafiki na Chad mwezi ujao huko Morocco.
Wanyama mwenye umri wa miaka 33 hajaichezea Harambee Stars kwa miaka minne tangu alipoamua kustaafu kuitumikia timu hiyo mwaka 2021 na sasa amerudi tena baada ya ushawishi wa McCarthy.
Kitendo cha Amrouche kumuita Kagere na McCarthy kumuita Wanyama kina maana kubwa na kinatupa darasa hapa nchini la kuheshimu na kuenzi mchango wa wachezaji ambao wamejitoa kwa muda mrefu kutumikia timu za taifa.
Kuna wakati wachezaji kama hao hata kama umri umeenda au hawako katika viwango bora, huwa wanahitajika kuwepo kwenye timu ili kusaidia kuwapa uzoefu wadogo zao ambao ndio wanaanza kuitumikia timu ya taifa kwa kipindi husika.
Hao sio aina ya wachezaji ambao wanatakiwa kuondolewa kwenye timu kienyeji na badala yake mchakato huo ufanyike katika namna ambayo mchezaji hatojisikia amedharauliwa au hajapewa heshima stahiki.
Kuiga mazuri sio dhambi hivyo nasi tunaweza kufuata nyayo za wenzetu Rwanda na Kenya kwa namna walivyofanya kwa Kagere na Wanyama.