Tizi la kina Morrison, Mugalu ni balaa!

Muktasari:

KOCHA mkuu wa Simba, Didier Gomes amewatengenezea programu maalum wachezaji wake kumi ambao hawajaenda kwenye timu za Taifa akiwemo Bernard Morrison na Chris Mugalu.

KOCHA mkuu wa Simba, Didier Gomes amewatengenezea programu maalum wachezaji wake kumi ambao hawajaenda kwenye timu za Taifa akiwemo Bernard Morrison na Chris Mugalu.

Gomes kama kawaida anaendelea na mazoezi na wachezaji wake kwenye uwanja wa Bunju, huku akisisitiza lengo kubwa ni kutaka wote wawe sawa tayari kwa mapambano na ndani na nje ya nchi.

Mwanaspoti lilishuhudia wachezaji Beno Kakolanya, Ally Salum, David Kameta, Ibrahim Ajibu, Ibrahim Ame, Said Ndemla, Benard Morrison, Pascal Wawa, Gadiel Michael na Cris Mugalu wakiwa wamechanganyika na wachezaji wa timu za vijana.

Kocha huyo akizungumza na Mwanaspoti lililotimiza miaka 20 sokoni, alisema lengo kubwa katika mazoezi yake ni kuhakikisha anawatengenezea ufiti wachezaji hao na kuwa na utimamu wa mwili muda wote.

“Nataka wachezaji hawa ambao hawapo na timu za Taifa wawe sawa na wale walio kwenye majukumu mengine, nawatengeneza ili kusiwe na utofauti,” alisema.

Gomes alisema katika mazoezi hayo asubuhi huwa wanafanya mazoezi magumu na kisha jioni anawapa mazoezi mepesi ili kuwafanya wachezaji wasichoke sana.

“Asubuhi nimewapa mazoezi magumu sana ili kuwawekea ufiti, jioni kama hivi nawapa mazoezi mepesi na kuchezea mpira sana kutokana na aina ya mazoezi waliyofanya asubuhi, lakini pia huwa wanaenda Gym.”

Mwanaspoti ambalo lilishuhudia mazoezi ya Jumanne jioni, liliona kocha huyo akiwataka wachezaji wake wachezee zaidi mpira kwa kufanya mazoezi mbalimbali.

Gomes pia aligawa timu mbili katika nusu uwanja kisha baada ya hapo aliwataka wachezaji wake wawe wanacheza kwa kugusa mara mbili mpira na baadaye aliwataka wacheze kwa uhuru zoezi likionekana kuwa zuri na wachezaji kufurahia.