Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tchetche Straika namba moja

MAISHA ni malengo na ndicho kinachomtofautisha binadamu mmoja na mwingine. Na ndiyo tofauti ya straika wa Azam, Herman Kipre Tchetche raia wa Ivory Coast na wachezaji wengine wazalendo wanaocheza nafasi kama yake.

Ni straika mwenye akili anayejua nini kimempandisha ndege kwa muda wa saa nane kutoka mjini Abidjan, Ivory Coast mpaka jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Alipoanza msimu malengo yake ilikuwa ni kufunga mabao 20 na amemaliza  na mabao 17. Anasikitika kwa hilo lakini bado ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Amewaacha mbali wanaomfuata kama Mrundi Didier Kavumbagu wa Yanga mwenye mabao 10, Paul Nongwa wa JKT Oljoro ana mabao nane sawa na Amri Kiemba wa Simba, Jerry Tegete wa Yanga na Hussein Javu wa Mtibwa Sugar.

Kavumbagu ndiye alikuwa tishio mzunguko wa kwanza ambao alifunga mabao saba lakini mzunguko wa pili makali yake yakapungua na akafunga mabao matatu tu na kumpa mwanya Tchetche kuzidi kupaa kileleni.

Tchetche anakumbukwa na mashabiki wa soka alipokuja kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam na timu yake ya taifa ya Ivory Coast kushiriki mashindano ya Cecafa.

Urefu wake ni wastani, lakini jamaa ana umbo lenye misuli mikubwa na amejazia vilivyo sehemu ya kifua, mikono, mapaja na vijumbulu hali inayomfanya kuwa tishio kwa mabeki wapinzani.

Ana sifa ya kupiga mashuti makali na aina ya mabao yake ni kupitia pembeni kwenye engo, kati na mbali.

Alipofanya mahojiano na Mwanaspoti, Tchetche anasema: "Namshukuru Mungu kwa kunifanya kuwa mfungaji bora, hii isingewezekana bila mchango wa wachezaji wenzangu, makocha na mashabiki," alisema Tchetche alipewa ruhusa ya kuondoka kabla ya mechi ya Jumamosi iliyopita na kocha wake mkuu, Stewart Hall pamoja na nyota wengine wa kigeni  wa klabu hiyo ambao ni pacha wake, Kipre Bolou, Wakenya; Jackins Atudo na Humphrey Mieno pamoja na Brien Umony wa Uganda.

 "Shukrani kwa Mwenyezi Mungu pamoja na wachezaji wenzangu na benchi zima la ufundi kwa ushirikiano wao,"anasema Tchetche, ambaye ni shabiki wa Manchester United.

"Nimeshindwa kitu kimoja tu,  kufikisha malengo niliyokusudia. Nilitaka kumaliza ligi na mabao 20 lakini sikukamilisha nimeishia hayo 17, nachukulia hali hiyo kama changamoto yangu kwa ajili ya msimu ujao kuona nafanya vizuri zaidi,"anaeleza Tchetche.

"Na nafikiri nimeshindwa kufikia malengo yangu kwa sababu ya majeruhi. Nilikuwa sina wakati mzuri mzunguko wa kwanza kwa sababu ya kuandamwa na majeruhi nikawa nacheza mechi mara kwa mara.

"Mzunguko huu wa pili ndiyo nimekuwa vizuri na kufunga mabao yote hayo, nashukuru sana,"anafafanua Tchetche ambaye wachezaji wenzake wamempa jina la Van Persie wakimfananisha na Mholanzi anayekipiga klabu ya Manchester United, Robin Van Persie.

Kocha anavyomzungumzia

Kocha wake, Hall anasema: "Tchetche ni mchezaji mzuri ana kipaji na nguvu za mpira  kiujumla ni msaada katika timu. Anacheza kitimu na kwa ushirikiano dhidi ya wenzake na anafuata maelekezo unayompa,' anafafanua Hall.

"Matatizo ya Tchetche ni kama ya washambuliaji wengine. Kuna sehemu ambazo ni rahisi kufunga huwa anakosa na nyingine ni ngumu kufunga yeye anafunga na kwangu nachukulia ni kawaida tu,"anasema Hall.

Nje ya soka

Tchetche ambaye alifika nchini akiwa anazungumza lugha moja tu ya Kifaransa, lakini sasa anaongea kwa kujitahidi Kiingereza na Kiswahili.

Anasema, anafurahia maisha ya Tanzania kwa sababu ameshakuwa mzoefu na mazingira:" Awali ilikuwa ngumu kwa sababu ya ugeni lakini sasa nimezoea."

Tchetche amekuwa mpenzi wa chapati na mchuzi, ugali na kuku na anasema anakifurahia aina hiyo ya msosi.

Awali akiwa Ivory Coast alizoea chakula chao cha asili cha Aloco. Aloco ni ndizi zinazokaushwa wao wanakula na samaki.

 Historia

Katika familia ya Tchetche wamezaliwa sita. Watatu kati yao ni wanaume na watatu ni wanawake.

Yeye ni uzao wa pili ambao wamezaliwa wawili pamoja na pacha wake, Michael Kipre Bolou. Kaka yao ni Oscar Kipre Patrick na ndugu zake wakike ni Kipre Larine, Kipre Josiane  na Kipre Andrea.

Anatoka katika kabila la Bete na amezaliwa na kukua katika kijiji cha Issia, Daloa, Ivory Coast.

Anasema ana mchumba, lakini amegoma kutaja jina lake na mtoto mmoja mwenye miaka mitatu, Kipre Astride.

 

HERMAN KIPRE TCHETCHE

Kuzaliwa: Desemba 16, 1987

Mahali: Issia, Daloa, Ivory Coast.

Klabu: JCA Treich-ville 1997-2011,

Azam FC 2011-

Taifa: Ivory Coast