Tchakei aanza tizi Ihefu

Muktasari:

  • Tchakei aliumia Aprili 6, mwaka huu, wakati Ihefu ilipoifunga KMC mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex na kumfanya kukosa michezo mitatu mfululizo ambayo ni dhidi ya Simba (Aprili 13), Singida Fountain Gate (Aprili 18) na Azam (Aprili 21).

Nyota wa Ihefu, Marouf Tchakei ameanza mazoezi mepesi na timu hiyo baada ya kukosekana kwa takriban wiki tatu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya kifundo cha mguu aliyoyapata katika mchezo wa 32 bora Kombe la Shirikisho dhidi ya KMC.

Tchakei aliumia Aprili 6, mwaka huu, wakati Ihefu ilipoifunga KMC mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex na kumfanya kukosa michezo mitatu mfululizo ambayo ni dhidi ya Simba (Aprili 13), Singida Fountain Gate (Aprili 18) na Azam (Aprili 21).

Akizungumza na Mwanaspoti, mchezaji huyo amesema ni jambo zuri kwake kurejea mazoezini japokuwa anaendelea na programu za benchi la matabibu.

"Ni vizuri kwangu kurudi na muda sio mrefu naamini naweza kucheza moja kwa moja. Kwa sasa bado sijaanza kujumuika na kikosi cha kwanza na wenzangu kwa sababu nimepewa siku kadhaa hadi pale madaktari watakapojiridhisha niko fiti asilimia 100," amesema.

Daktari wa timu hiyo, Shima Shonde amesema hawatafanya haraka nyota huyo kurudi uwanjani kwani majeraha aliyopata  yanahitajika uangalifu wa hali ya juu ndio maana wakampa programu binafsi kabla ya kujiunga na wenzake.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime amesema licha ya umuhimu wa mchezaji huyo katika kikosi, lakini hawatakuwa na haraka ya kumtumia kwa michezo ijayo ili kumpa nafasi ya kupona vizuri na kurejea katika ubora wake.

"Mchezo wetu ujao wa robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Mashujaa tutakaocheza Mei Mosi tutaangalia na fitinesi yake kwa ujumla kabla ya kumtumia, ila kama nilivyosema hapo awali sio rahisi kucheza kwa sababu tunahitaji apone vizuri," amesema Maxime.