TBC kuongeza burudani Kombe la Dunia 2022
Shirika la utangazaji la TBC, limezindua rasmi mbio za kuonyesha michezo 28 kwa upande wa runinga na michezo 64 kwa upande wa radio, michuano ya Kombe la Dunia inayofanyka kuanzia leo Novemba 20 mpaka Disemba 18, 2022 nchini Qatar.
Akizungumza na Mwanaspoti Mkurugenzi wa Masoko wa TBC, Dafrosa Kimbori ameeleza kwa kina haki walizozipata kurusha matangazo hayo na endapo litatokea tukio sio la dharura mechi hazitosimama.
“TBC kama chombo cha taifa leo tumejipanga kwa kuanza na uzinduzi maaluumu baada ya kupata haki ya kurusha michuano hii ya Kombe la Dunia kwa upande wa TBC1 kuonyesha mechi 28 na kwa TBC taifa tutangaza zote 64 kwa ubora wa hali ya juu.” amesema na kuongeza.
“TBC kama chombo cha taifa tuwahakikishie watazamaji na wasikilizaji kupata uhondo wa michuano hii na ikiwa imetokea tukio la kitaifa kama sio la dharura tutasubiri mechi iishe na kama ni la dharura linatulazimika kupeleka habari haraka tutatumua mitandao yetu ya kijamii kufikisha hilo tukio la kitaifa kwa haraka zaidi.” amesema kimbori.
Mtangazji wa TBC, Evance Muhado ameeleza kuwa ni kitu kikubwa kwao kuonyesha michuano hii ya Kombe la Dunia na maandalizi yao yalianza mapema mwezi mmoja kabla ya michuano hii.
“Ni kitu kikubwa sana na heshima kwa nchi na sio mara ya kwanza kwa TBC kuonyesha Kombe la Dunia tangu 2010 mechi 28 ni nyingine japo nyuma tulikuwa tunaonyesha mechi chache na sisi kama tupo tayari watazamaji na wasikilizaji wajiandae leo tunaenda kusimamisha nchi.” amesema Muhando.
Michuano ya Kombe la Dunia itaonyeshwa kwenye chaneli ya taifa inayopatikana bure katika visimbuzi vyote vinavyopatikana Tanzania na radio ya TBC taifa.