Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Taifa Stars yaipa mzuka kinoma Serengeti Boys kupindua meza kwa Angola

Muktasari:

  • Taifa Stars ilifuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Misri ikiwa ni mara ya pili kwake kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 1980

Dar es Salaam. Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 'Serengeti Boys' inaamini bahati iliyoibeba timu ya taifa ya wakubwa 'Taifa Stars' kwa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu dakika za mwishoni, itawabeba kwenye mchezo wa mwisho wa kundi A la Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri huo (AFCON U17) dhidi ya Angola.

Stars iliyokuwa Kundi L la mashindano ya kufuzu fainali za AFCON ilisubiri hadi mechi ya mwisho dhidi ya Uganda iliposhinda mabao 3-0 na kisha kubebwa na sare ya baina ya Cape Verde na Lesotho, ili kufuzu fainali hizo.

Hali kama hiyo ndio imeikuta Serengeti Boys ambayo inapaswa kupata ushindi wa angalau mabao 4-0 na kisha kuombea Uganda ifungwe na Nigeria kwa kipigo cha angalau kuanzia mabao 3-0 ili kutinga hatua ya nusu fainali na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la vijana chini ya umri wa miaka 17 zitakazofanyika Brazil mwezi Oktoba.

Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo alisema baada ya kufanya vibaya katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Nigeria na Uganda, anaamini maajabu ya Taifa Stars yanaweza kutokea upande wao ikiwa watashinda mechi ya mwisho dhidi ya Angola.

"Tunaamini nafasi ipo. Timu ya taifa ilifuzu vipi kwenda Fainali za Mataifa ya Afrika? Ilipenya kwa kutegemea pia matokeo ya mechi nyingine na lengo likatimia. Huu ni mchezo wa mpira lolote linaweza kutokea.

Tuna mechi moja ya kucheza. Jambo zuri kwenye hii mechi ya mwisho ni kuwa bado tuna nafasi ya kupita ikiwa tutapata ushindi, na Uganda atapoteza.

Tunataka kusaka ushindi kesho halafu baada ya hapo tutaangalia mechi ya Uganda ikoje," alisema Mirambo.

Mirambo alisema hakuna kinachoshindikana kwenye mchezo wa mpira wa miguu hivyo watapambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na ikiwezekana kufuzu hatua inayofuata.

Nahodha wa Serengeti Boys, Mourice Abraham alisema hawana presha na wanajiandaa vyema kwa ajili ya mchezo wa kesho.

"Unapojikwaa unatakiwa unyanyuke kwa haraka na kuendelea na safari hivyo sisi kwa upande wetu tunatazama mbele na tuko vizuri kwa ajili ya mchezo wa kesho," alisema Abraham.