Tabwe atibua chereko kwa Prisons

Muktasari:

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera, alifanya mabadiliko ya kiufundi katika kikosi chake ambayo yalikuwa na faida kubwa katika mchezo huo uliotawaliwa na ubabe dakika zote tisini.

Mbeya. Mabadiliko ya benchi la ufundi, ubabe wa wachezaji wa Prisons na Yanga ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera, alifanya mabadiliko ya kiufundi katika kikosi chake ambayo yalikuwa na faida kubwa katika mchezo huo uliotawaliwa na ubabe dakika zote tisini.

Zahera alimuinua katika benchi mchezaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Tambwe ambaye alikuwa shujaa wa mchezo huo, baada ya kufunga mabao mawili.

Kocha huyo alifanya uamuzi mgumu wa kumtoa beki na nahodha, Juma Abdul na kumuingiza Tambwe. Pia Thabani Kamusoko aliingia badala ya Feisal Salum, Matheo Anthony alichukua nafasi ya Maka Edward. Mabadiliko hayo yaliongeza uhai kwa Yanga ambayo ilicheza kwa nguvu kwa kulishambulia lango la Prisons kutaka mabao.

Kamusoko alitumia uzoefu wake katika eneo la kiungo kuchezesha timu huku akipenyeza pasi za mwisho kwa akina Ibrahim Ajibu aliyekuwa mwiba kwa mabeki wa Prisons.

Yanga ikiwa nyuma kwa bao 1-0, ilipindua matokeo na kupata ushindi wa mabao 3-1 na kuendelea kubaki kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 38 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 33.

Tambwe ambaye msimu uliopita alikosa takribani mechi zote za Ligi Kuu, msimu huu amerejea katika kikosi ingawa hajapata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Prisons ilitangulia kupata bao lililofungwa na Jumanne Elfadhili kwa penalti dakika ya 45 kutokana na makosa ya beki Andrew Vincent ‘Dante’ aliyefanya madhambi ndani ya eneo la hatari langoni mwake.

Mwamuzi Meshack Suba wa Singida ambaye alikuwa akizongwa mara kwa mara na wachezaji wa timu zote, aliwapa kadi nyekundu Mrisho Ngassa wa Yanga na Laurin Mpalile wa Prions dakika 49 kwa utovu wa nidhamu.

Ngassa alipewa kadi hiyo baada ya kumpiga kichwa Hassani Kapalata na Mpalile alimsukuma mwamuzi huyo, baada ya kutokea vurugu baina ya wachezaji wa pande hizo.

Kocha wa Prisons, Mohammed Abdallah ‘Bares’ alisema hawezi kutoa lawama kwa wachezaji licha ya kupoteza mchezo huo ambao Prisons ilionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

Kipigo hicho kimeifanya Prisons iliyocheza mechi 15 kujichimbia shimo, ikibaki katika nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 10 sawa na Biashara United inayoshika mkia.