Straika Prisons azitaka Simba, Yanga

STRAIKA wa Tanzania Prisons, Ismail Mgunda amesema licha ya kuwa miongoni mwa wachezaji waliofunga ‘hat trick’ kwenye Kombe la Shirikisho (ASFC) lakini msimu huu anakitamani sana kiatu cha mfungaji bora, huku akitamba wanamsubiri yeyote hatua inayofuata.
Mgunda ambaye ni msimu wake wa kwanza kucheza Prisons, juzi aliiongoza timu hiyo kuichakaza mabao 7-1 Misitu FC, huku mwenyewe akiingia kambani mara tatu na kuondoka na mpira wake.
Nyota huyo ambaye aliwahi kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini katika kikosi cha Jomo Cosmos amekuwa na msimu bora na uhakika wa namba kwenye timu hiyo pamoja na ugeni wake.
Akizungumza na Mwanaspoti, alisema anafahamu ugumu lakini umuhimu wa kutwaa tuzo itamfungulia zaidi milango katika kipaji chake akibainisha siri kubwa ya mafanikio ni ushirikiano na kujituma. “Natamani nafasi hiyo, ndiyo maana nikipata nafasi nafunga mabao, lakini ushindani najua upo ila timu imefuzu na tunaomba yeyote aje matarajio ni kuona Prisons inatwaa taji hili kwa mara ya kwanza na lolote linawezekana,” alisema Mgunda.
Kuhusu matokeo ya ligi, nyota huyo alisema bado hawajawa na matokeo mazuri na wanapaswa kukaza kwenye mechi za lala salama kuhakikisha hawachezi tena ‘play off’ kama ilivyokuwa msimu uliopita.