Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Stella Abidjan walitufunga kihalali kombe la Caf 1993

Masatu

Muktasari:

Kwa upande wa mafanikio, mchezaji huyo anamshukuru Mungu na kusema amepata ya kutosha kutokana na kucheza soka ndani na nje ya nchi. Masatu anasema alinufaika zaidi baada ya kutoka nje ya Tanzania.

Makala haya ya Masatu yanaendelea yalipoishia, wiki mbili zilizopita mchezaji huyo alipozungumzia mafanikio aliyoyapata katika soka, pamoja na hilo Masatu anauzungumzia mchezo wa Fainali ya Kombe la CAF uliopigwa jijini Dar es Salaam mwaka 1993. Endelea...

Kwa upande wa mafanikio, mchezaji huyo anamshukuru Mungu na kusema amepata ya kutosha kutokana na kucheza soka ndani na nje ya nchi. Masatu anasema alinufaika zaidi baada ya kutoka nje ya Tanzania.

“Mafanikio ni mengi sana kupitia soka ukiachana na kujulikana, nimefanya mambo mengi kwa fedha niliyoipata ndani na nje ya nchi, niliweza hata kujenga nyumba.”

Mechi na Stella Abidjan

Mwaka 1993, Simba ilicheza fainali za Kombe la Caf (sasa Kombe la Shirikisho) na timu ya Ivory Coast ya Stella Abidjan jijini Dar es Salaam baada ya kutoka sare ugenini.

Mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa (siku hizi Uwanja wa Uhuru) mgeni rasmi alikuwa ni Rais wa Tanzania wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi.

Ili kuweza kufanya vizuri katika mchezo huo, mfadhili wa Simba, Azim Dewji aliwaahidi wachezaji wa timu hiyo magari aina ya Toyota KIA kama wangeshinda mchezo huo na kutawazwa kuwa mabingwa wa Afrika wa Kombe la Caf.

“Ni kweli tuliahidiwa magari aina hiyo lakini hatukupewa badala yake tulipewa magari ya aina ya Toyota Corolla, kwa kuwa tulipoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 2-0,” anakumbuka.

Masatu anasema kuwa hawezi kuisahau siku hiyo katika maisha yake kwa kuwa hakutegemea kama wangefungwa lakini walizidiwa mchezo na wenzao wa Stella Abidjan na kufungwa kihalali bila ya hujuma yoyote.

“Pamoja na kwamba tulipewa magari hayo aina ya Corolla lakini baadhi ya wachezaji tuliambiwa kuwa tuliuza mchezo ule baada ya kufungwa na mchezaji wa Stella Abidjan aitwaye Boli Zozo aliyepachika mabao yote,” anasema Masatu.

Masatu anawataja wachezaji waliotuhumiwa kuuza mchezo huo ni Marsha, Mohammed Mwameja na yeye mwenyewe pamoja na wengine.

”Dewji alilazimika kutupa Corolla ili kufuta imani ya watu kuwa tumehujumu timu kwa kuwa alikuwa akituamini ingawaje mpaka leo hii watu hawakubali ukweli kwamba tulizidiwa, hatukuuza mechi ile,” anasema Masatu

Kufundisha academy ya Arsenal

Wakati Masatu alipokuwa Indonesia alipata bahati ya kufundisha kituo cha Arsenal cha kulea na kukuza vipaji vya vijana akiwa kama kocha.

“Nimefundisha kwa mafanikio makubwa kwani kituo chetu kiliweza kutwaa nafasi ya tatu kwenye mashindano makubwa ya Indonesia.

“Kituo hicho kipo chini ya Klabu ya Arsenal, hivyo kila mwaka wanakuwa na mashindano yao kuanzia watoto wenye umri wa miaka minane, 12 na 14, mpaka naondoka nilikuwa kocha wa kituo hicho,” anasema.

Leseni ya Fifa

Masatu anabainisha kwamba ana leseni ya ukocha wa Daraja A kimataifa inayotambuliwa na Shirikisho la soka la Kimataifa (Fifa) aliyoipata akiwa Indonesia ingawa tangu arudi hapa nchini hajawahi kuifanyia kazi.

“Mimi ni kocha na nina leseni inayotambulika na Fifa na niliwapalekea TFF wakaniambia mpaka niwe mwanachama wa chama cha makocha nchini, ambao pia waliniambia mpaka nisomee kozi nyingine ili nipate cheti, nilishindwa kuwaelewa nina leseni ya Fifa halafu nisome cheti cha kazi gani?

“Kila mwaka Fifa wanatoa nafasi za makocha wa ngazi hiyo ambazo hapa hazitangazwi ipasavyo na ndiyo maana wanasema Tanzania ina makocha wachache wenye leseni hizo lakini si kweli, TFF wanapaswa kupanua wigo sasa ili makocha wasome zaidi na kuwa na leseni kama hizi,” anasema.

Mawakala/mikataba ya wachezaji

Anasema kuwa mawakala wengi si wakweli ndiyo maana kunakuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wachezaji kuwa wanadhulumiwa haki zao.

“Mpaka mchezaji anafanikiwa kucheza Ulaya anapitia kwenye mikono ya watu wengi, anaanza na wakala aliyemuunganishia hapa nchini na wao wanakuwa na mawakala wao, hivyo ni kama watu watatu wanahitaji fedha hiyohiyo.

“Ndiyo maana mkataba wa kwanza kwa wachezaji wengi unakuwa ni wa hasara sana lakini kama mchezaji ni mjanja hawezi kuingia hasara, anatakiwa aombe kuuona mkataba wake kwanza na auelewe ndipo asaini, kwangu ilikuwa tofauti kwani sikupitia kwenye mikono ya mawakala, ukiwa makini nje kuna masilahi mazuri,” anasema.

Viwango vya wachezaji wa Bongo

Masatu haamini kama viwango vya wachezaji nchini vimeshuka ila anadai kuwa hakuna kocha anayetambua matatizo ya mchezaji mmoja mmoja.

“Nilishangaa sana nilivyorudi nchini na kuambiwa kwamba Tanzania haina wachezaji, mara viwango vimeshuka, hilo si kweli kuna wachezaji wengi hapa tena wazuri ila makocha ndiyo hawatambui matatizo ya wachezaji haraka.

“Ukiwa kama kocha unatakiwa kumtambua mchezaji wako, kama mwanzo alikuwa anafanya vizuri na sasa anafanya vibaya ni lazima ujiulize na kukaa naye ili kujua tatizo lake ni lipi, kocha hatakiwi kuwa mkali, kwani wachezaji wengi hujaa hofu pale wanapokaripiwa hivyo itakuwa ni vigumu kujua matatizo yao.

“Lakini pia viongozi wa timu wawe watu wa kuzunguka ama kwenda kwenye mazoezi ya timu zao, viongozi na makocha hawatakiwi kuwa wabaguzi, mara nyingi mchezaji unatambua tatizo lake mazoezini na si kwingineko, wachezaji wana viwango na wapo wengi wanaojua, tatizo ni hilo tu,” anasema Masatu.

Mazoezi ya gym na beach

Timu nyingi zinapoanza msimu mpya hapa nchini huanza mazoezi ya beach (ufukweni) na kunyanya vitu vizito, gym, Masatu anasema kiafya mazoezi hayo si mazuri kwa wachezaji wanaotoka mapumzikoni.

Anasisitza kwamba kocha anatakiwa awape mazoezi mepesi ya uwanjani kabla ya kwenda beach na gym.

“Mazoezi ya gym na beach hayana tofauti, ni ya kuongeza nguvu, kama kocha amesoma atakuwa anaelewa madhara ya kumwanzishia mchezaji mazoezi magumu, mchezaji akitoka mapumziko anatakiwa aanze mazoezi mepesi kwa wiki moja au mbili.

“Mchezaji anapelekwa gym au beach endapo utamuona hana nguvu za kutosha, si sahihi kumpa mazoezi hayo kwani kazi yake ni mchezaji si wanyanyua vyuma,’’ anasema.

anzo uwanjani, kocha anatakiwa aanze kwa dakika chache halafu apenge taratibu kulingana na siku alizojiwekea kwa wiki hizo kabla ya kwenda gym au beach. anasema.

Anataja sifa za kocha bora

“Ogapa sana kuwa na kocha mwenye sifa hizi, awe amecheza, amesomea mpira, anafundisha mpira na upeo wa kumsoma mchezaji mmoja mmoja, kocha wa aina hii ni mzuri sana na huwezi kumdanganya kwa lolote.

“Makocha kama hawa wapo wengi Tanzania ila wanadharaulika, hawathaminiwi na wala hawapewi nafasi ya kufundisha na hiyo inatokana na chuki tu za baadhi ya viongozi,” anaeleza.

Uchawi katika soka

Anasema “Siwezi kusema upo au haupo kwani kila mmoja ana imani, nikiwa mchezaji mambo mengi yalikuwa yakifanyika na huwezi kumkataza mtu kufanya kwa sababu anaamini kuwa akifanya hivyo atashinda.

Ila nilichokuwa nakiamini na kushiriki kama kuna kusoma dua nilishiriki vizuri kwani hiyo ni ibada.”

Kujihusisha na Simba

Tangu amerudi nchini, Masatu hajajihusisha na timu yake ya zamani ya Simba.

“Wachezaji wa zamani hawajihusishi na timu walizozichezea ni kwa sababu hawathaminiwi, mchango wao hauonekani hiyo si kwa klabu tu, thamani ya mchezaji inatakiwa ianze kuonekana ngazi ya taifa ndipo klabu zifuate vinginevyo itakuwa ni kupiga kelel.

Masatu anahoji anasisitiza kwamba wachezaji wengi wamecheza timu ya taifa lakini taifa halina mchango wowote kwao na kusema ni jambo linalokatisha tamaa kwani wachezaji na viongozi wanatakiwa kuungana na kutoa mchango yao.

“TFF wanatakiwa kutuunganisha na siyo sisi kwenda kuwaomba wao, kuunganisha ni pamoja na kutupa kadi za uanachama ili hata kama mchezaji wa zamani anaenda kuangalia timu yake ya taifa akionyesha kadi aruhusiwe kuingia uwanjani pia watuite pamoja wasikilize mawazo yetu, lakini mbaya zaidi wanashindwa hata kutusiadia katika matatizo.

“Wakifanya hivyo watakuwa wameturudisha kwenye mfumo wa soka na mawazo yetu yatakuwa sawa,” anafafanua Masatu

Mechi anayoikumbuka

“Nakumbuka mechi Simba na Yanga iliyochezwa miaka ya 90 ilikuwa ngumu sana kwa kuwa tulipaniana sana, kila mmoja akitaka kumfunga mwenzake lakini mwishowe tulitoka sare ya bila kufungana,” anasema Masatu.

Kizota alikuwa msumbufu

Masatu anamtaja mchezaji wa zamani wa Yanga, marehemu Said Mwamba ‘Kizota’ kwamba ndiye mchezaji pekee aliyemsumbua uwanjani.

“Jamaa alikuwa na kiwango cha hali ya juu, ukiachana na kufundishwa na kocha wake lakini alikuwa na uwezo binafsi.

“Nilikuwa napata wakati mgumu sana kumkaba ingawa hata mimi nilijituma lakini nikiona amenizidi ujanja nilikuwa napata na changamoto kubwa ya kutafuta mbinu ili niweze kumdhibiti, Mungu amrehemu kwa kweli, sijui kama watapatikana wachezaji wengine kama yeye,” anasema.

Pamba kuna tatizo gani?

Msimu uliopita, Masatu alikuwa kocha mkuu wa timu ya Pamba ambayo amewahi kuichezea, timu hiyo ilikuwa inashiriki Ligi Daraja la Kwanza lakini haikufanya vizuri ikashuka daraja.

“Pamba haikunifurahisha sana, uwezo wao wa uchezaji haukuwa mzuri walicheza chini ya kiwango, uongozi ndiyo tatizo na ulikuwa na mzigo mkubwa kwani haukuwa na fedha hivyo mazingira ya timu yalikuwa mabaya, viongozi wa Pamba wanatakiwa kujipanga kwa muda mrefu ili kurudisha hadhi.

“Pamoja na kwamba Pamba ilikuwa na matatizo hayo lakini TFF kupitia waamuzi wao ndiyo wanaochangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa soka nchini, kwani waamuzi hawatendi haki, wachezaji ni wazuri ila maamuzi yanayotolewa na waamuzi yanawaumiza wachezaji,” anasema.

Tofauti ya Ligi Kuu Bara

“Ligi ya sasa ina ushindani mkubwa na wachezaji wanapata fedha nyingi lakini bado waamuzi hawafuati sheria 17 za soka, naomba watakaobainika na makosa wachukuliwe adhabu kali za kisheria, waamuzi wanachezesha kwa mapenzi zaidi,”.

Maisha nje ya soka

Masatu alikaa Indonesia kwa miaka 13 huku akiacha familia yake nchini, lakini aliporejea alijikuta akitengana na familia yake akiwamo mtoto wake wa kike ambaye anaishi na mama yake.

“Ni mengi yametokea ambayo siwezi kuyasahau maishani mwangu, kikubwa namshukuru Mungu anaendelea kunipigania naishi na ndugu zangu Mbagala baada ya kutengana na mke wangu.

“Sitegemei kurudi Indonesia kwa sasa, kwanza hata familia yangu haiwezi kuniruhusu na mpaka hati yangu ya kusafiria wameishikilia wao, yote hayo ni kutokana na mambo yaliyotokea katika familia yangu,” anasema.