Stars tayari kushiriki Chan

Muktasari:

Timu ya Taifa Stars leo Januari 13, 2020 jioni imefanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kesho alfajiri itasafiri kwenda nchini Cameroon kushiriki michuano ya Chan.

KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ leo jioni kimefanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa tayari kwa michuano ya Chan inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 16 nchini Cameroon.

Katika mazoezi ya leo Kocha mkuu wa timu hiyo Ettiene Ndayiragije alitoa mazoezi mepesi kwa wachezaji 25 wa timu hiyo waliohudhuria mazoezi hayo wakianza kwa kunyoosha viungo kisha kukimbia na kuchezea mpira kitimu ambapo alitenga timu mbili na kuanza kucheza mechi.

Mwisho wa mazoezi hayo wachezaji wote walioshiriki walienda nje ya uwanja kulipokuwa na pipa zenye barafu na kuingia mule kwa awamu ambapo kila mchezaji alikaa ndani ya pipa kwa dakika zisizopungua tano.

Sambamba na hilo Nahodha wa kikosi hicho John Bocco na beki Erasto Nyoni hawakuonekana mazoezini hapo huku mabeki wengine Ibrahim Ame na Dickson Job, golikipa Aboutwalib Msheri na mshambuliaji kinda Omar Omari wakikaa jukwaani kwa kuwa ni majeruhi.

Wachezaji walioshiriki mazoezi ya leo ni Juma Kaseja, Aishi Manula, Daniel Mgore, Israël Mwenda, Yassin Mustapha, Edward Manyama , Paschal Gaudence, Shomari Kapombe, Carlos Protos, Bakari Mwamnyeto, Zuberi Dani, Said Ndemla, Feisal Salum, Ayoub Lyanga, Khelfinnie Salum, Deus Kaseke, Yusuph Muhilu, Farid Mussa, Adam Adam, Baraka Majogoro, Rajab Athuman, Samuel Jackson, Ditram Nchimbi, Lucas Kikoti na AbdulRazack Hamza.

Timu hiyo itasafiri  saa 7:00 za usiku kuelekea nchini Cameroon kwa usafiri wa ndege na inatarajia kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere saa 6:00 usiku tayari kwa safari hio.

Jitihada za kupata kikosi kamili kitakachosafiri kuelekea nchini Cameroon bado zinafanyika.