Stars kuwamaliza Malawi kesho

Muktasari:
KOCHA mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameanza kutengeneza mbinu za kuwamaliza Malawi katika mchezo wao wa kirafiki utakaochezwa kesho Jumapili saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
KOCHA mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameanza kutengeneza mbinu za kuwamaliza Malawi katika mchezo wao wa kirafiki utakaochezwa kesho Jumapili saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Katika mazoezi ya wiki hii katika Uwanja wa JK Youth Park, Kim alikuwa anawapa wachezaji wake mazoezi ya mbinu kuhakikisha wanaenda kupata ushindi katika mchezo huo.
Mwanaspoti ambalo lilikuwepo uwanjani hapo lilishuhudia, Kim akipanga wachezaji wake katika makundi tofauti na kuwataka wacheze kwa kupeana nafasi ya kusonga mbele na kupiga zaidi pasi za haraka haraka huku kukiwa na misogeo.
Baada ya kuona zoezi hilo aligawa timu kwa pande mbili na kutaka wafanye kwa usahihi na wachezaji wake hawakumuangusha katika zoezi hilo kwani walikuwa wanafata kwa ufasaha.
Kim, pia aligeukia upande wa washambuliaji mbele kumpanga Kibu Denis, Yohana Mkomola, Abdul Suleiman na John Bocco wawe makini pindi wanapopewa pasi za mwisho na kufunga.
Wakati Kim akiwasimamia washambuliaji hao, makocha wasaidizi Seleman Matola na Juma Mgunda wao walikuwa makini katika kuangalia maeneo ya ulinzi na viungo washambuliaji kuhakikisha hawakai na mpira kwa muda mrefu bali wanaipeleka kwa washambuliaji.
Akizungumzia mchezo huo wa Malawi, Mgunda alisema; “Wachezaji wapo vizuri wote ukizingatia wametoka katika timu zaohuku Ligi Kuu ikiwa inaendelea, tunachoangalia kwasasa ni kuwapa mbinu tu za kwenda kwenye mchezo.”
“Malawi ni timu nzuri na kitakuwa kipimo kizuri kwetu kwa sababu wapo katika kipindi bora na sisi hatujacheza nao kwa muda mrefu.”
“Kuhusu Mbwana Samatta ana matatizo ya kifamilia, sio yeye bali kwenye familia kwahiyo kwasasa hayupo lakini kwa siku tatu zijazo atajiunga na wenzake, Msuva na yeye hayupo kwa sababu yupo katika majukumu ya klabu yake, wana mechi ngumu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kama atakuja inaweza ikawa siku moja kabla ya mchezo wetu,” alisema Mgunda.
Wachezaji waliokuwepo katika mazoezi ya Stars ni Wachezaji wengine waliokuwepo ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Edward Charles, Israel Patrick, Juma Kaseja, Metacha Mnata, Bakari Mwamnyeto na Erasto Nyoni.
Wengine ni Meshack Abraham, Dickson Job, Ayoub Lyanga, Nickson Kibabage, Kennedy Juma, Mzamiru Yassin,Mudathir Yahya, Salum Abubakari,Yusuph Mhilu, Feisal Salum, John Bocco, Kibu Denis, Abdul Suleiman na Yohana Mkomola.