SITA WAPIGWA CHINI YANGA

Muktasari:
Amefanya mabadiliko katika nafasi sita za kikosi cha kwanza kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikionekana ni kujikita kwenye njia ya ubingwa ambao pia Simba wana nafasi ya kuubeba. Ingawa haijawekwa wazi, lakini inadaiwa kuwa baadhi ya mabadiliko hayo yanalenga kuingiza wachezaji wenye mzuka wa ubingwa na wasio na visingizio haswa katika kipindi hiki kigumu ambacho viongozi wanalia na ukata klabuni.
YANGA ina mechi tano mezani ambazo kwa namna yoyote ile wanapaswa kushinda kama wanataka kutetea ubingwa wao, lakini Kocha George Lwandamina amepangua kikosi hicho na kuweka kando baadhi ya mastaa waliozoeleka.
Amefanya mabadiliko katika nafasi sita za kikosi cha kwanza kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikionekana ni kujikita kwenye njia ya ubingwa ambao pia Simba wana nafasi ya kuubeba. Ingawa haijawekwa wazi, lakini inadaiwa kuwa baadhi ya mabadiliko hayo yanalenga kuingiza wachezaji wenye mzuka wa ubingwa na wasio na visingizio haswa katika kipindi hiki kigumu ambacho viongozi wanalia na ukata klabuni.. .
KAKOLANYA/DIDA
Benno Kakolanya, ambaye awali alikuwa hapati nafasi amemuondoa Deo Munishi ‘Dida’ aliyecheza mechi nyingi kikosini hapo kuliko kipa mwingine msimu huu.
Katika mzunguko wa kwanza Kakolanya alicheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Prisons ugenini, akicheza penalti lakini mzunguko wa pili akarudishwa tena golini dhidi ya timu hiyo hiyo ukiwa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA.
KESSY/ABDUL
Kulia nako kuna sura mpya. Juma Abdul ambaye katika mechi chache zilizopita alikuwa majeruhi, amemuachia nafasi Hassan Kessy na kwa sasa anaonekana kuwa katika kiwango bora na kulishawishi benchi la ufundi kumpa nafasi katika kikosi cha kwanza.
Beki ya kushoto Haji Mwinyi Mngwali amedumisha kiwango chake na kubaki kuwa chaguo la kwanza huku mkongwe Oscar Joshua akimsubiri katika benchi.
CANNAVARO/BOSSOU
Nahodha wa kwanza katika kikosi hicho Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amerudishwa na Vincent Bossou amekaa kando kwa sababu mbili, majeruhi pamoja na kususa akidai chake.
Kelvin Yondani ndiye anayecheza sasa sambamba na Cannavaro huku Andrew Vincent ‘Dante’ akisubiri katika benchi ingawa yuko katika kiwango bora sana.
MAKAPU/ZULU
Kuumia kwa Justine Zulu kumemnufaisha Said Juma Makapu, ambaye sasa ndiye anayechezeshwa nafasi ya kiungo mkabaji ingawa Zulu amesharudi na kuanza mazoezi na wenzake.
KAMUSOKO/NIYONZIMA
Kiungo mchezeshaji wa juu majukumu yapo chini Thaban Kamusoko akimuweka kando Haruna Niyonzima aliyekuwa na majeruhi, lakini Kamusoko akipandishwa juu baada ya awali kubeba jukumu la kiungo ya chini ingawa uamuzi huo wa kucheza juu kidogo umetokana na ujuzi wa kupiga pasi za mwisho na wepesi wa kushuka kusaidia ukabaji wakati timu ikishambuliwa.
Winga Simon Msuva amejihakikishia nafasi yake katika kikosi hicho kutokana na kiwango bora msimu huu, kinachotokana na mazoezi makali kikosini na yale binafsi anayoyafanya.
MWASHIUYA/KASEKE
Winga Geofrey Mwashiuya naye amechomoza katika kikosi hicho akiwabadili Deus Kaseke na Emanuel Martin ambao, ndiyo waliokuwa wakipishana awali.
Faida ya Mwashiuya katika nafasi ni matumizi yake ya mguu wa kushoto ambayo yanampa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza huku akiwa na nguvu na mbinu za kuwabana na kuwakimbia mabeki kwa kasi ya ajabu.
TAMBWE NA CHIRWA TU
Kurudi kwa Amissi Tambwe kumemfanya sasa kucheza sambamba na Obrey Chirwa huku staa huyo wa Burundi akionekana kuwa sawa sawa baada ya kucheza mechi yake ya kwanza na kufunga bao la ufundi kwa kichwa dhidi ya Prisons.
MECHI ZILIZOSALIA
Yanga katika kujipanga na ubingwa imebakiza mechi tano ikicheza Aprili 6 dhidi ya Prisons, itarudi tena uwanjani Mei 9 ikiwakaribisha Kagera Sugar kisha kukutana na Mbeya City Mei 13 na pia kukutana na Toto African Mei 16 zote wakicheza nyumbani kisha kumalizia ugenini Mei 20 dhidi ya Mbao FC. Mechi hizo zinatajwa kuwa ndio zimeshikilia ubingwa wa Yanga.
MAZOEZINI JANA
Donald Ngoma na Vincent Bossou hawakufanya mazoezi ya mwisho jana kabla ya timu kusafiri kwenda Mwanza kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Mbao FC.
Daktari wa timu hiyo, Edward Bavu aliliambia Mwanaspoti kuwa; “Bossou ameanza matibabu juzi baada ya kuumia nyuma ya goti hivyo, hatoweza kucheza mechi ya Mbao lakini anaweza kucheza mechi zijazo.
Ngoma anaendelea vizuri na kuanzia kesho (leo) anaweza akajiunga na wenzake,” alisema.
Bavu alibainisha kuwa wachezaji waliobaki hawana majeraha huku kiungo wao mkata umeme, Justine Zullu akiwa amepona.