Simba yazidi kuikacha Yanga

Kiungo wa Simba, Muzamiru Yassin (kulia) akishangilia bao lake na Mohamed Ibrahim wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Toto Africans uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru. Simba ilishinda 3-0. Picha na Omar Fungo
Muktasari:
- Simba iliitandika Toto kwa mabao 3-0 kwenye pambano lililopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam
BAADA ya kupata ushindi mnono wa mabao 6-2 dhidi ya Kagera Sugar, Yanga ilipanda hadi nafasi ya pili na mashabiki wake kuamini bado kidogo iwakamate watani zao Simba waliopo kileleni mwa Ligi Kuu Bara.
Lakini kama ilikuwa haifahamu ni kwamba Simba ya sasa sio timu ya mchezo mchezo, kwani jana Jumapili iliandikisha ushindi wake wa tisa msimu huu kwa kuitungua Toto Africans ya Mwanza na kuzidi kuwaacha mbali watani zao hao.
Simba iliitandika Toto kwa mabao 3-0 kwenye pambano lililopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam huku ikishuhudia Mzamiru Yasin na Laudit Mavugo wakifunga na kufanya kila mmoja afikishe mabao manne mpaka sasa katika ligi.
Mzamiru alifunga mabao mawili na Mavugo moja na kuwafanya wawanase kilaini mastraika wa Yanga Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Obrey Chirwa waliokuwa wamewatangulia kwenye orodha ya wafungaji mabao wa Ligi Kuu.
Mzamiru alifunga bao la kwanza dakika chache kabla ya mapumziko akimalizia pande zuri la Frederick Blagnon kabla ya Mavugo aliyeingia kipindi cha pili kumpokea Blagnon aliyeumia kuongeza la pili dakika ya 52.
Wakati Toto ikicharuka kutaka kurejesha mabao hayo Mzamiru aliongeza bao la tatu lililowakata maini akimalizia kona tamu iliyopigwa na Janvier Bokungu na kutengenezewa vizuri mpira na Jamal Mnyate kabla ya kufunga kwa shuti kali.
Ushindi huo umeifanya Simba kujichimbia kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 11, ikiiacha Yanga na Stand United zilizopo nyuma yake kwa pointi nane, kwani zenyewe zina pointi 21 kila moja.
Simba: Vincent Angban, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein, Juuko Murshid, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mzamiru Yasin, Frederick Blagnon/ Laudit Mavugo, Mwinyi Kazimoto/Jamal Mnyate na Mohammed Ibrahim.
Toto: Mussa Kirungi, Yusuf Mgeta, Hamim Abdallah, Jafar Mohammed, Carlos Protas/Ramadhani Malima, Yusuf Mlipili, Soud Mohammed/Frank Sekule/ William Kimanzi, Salum Chuku, Wazir Junior, Reliant Lusajo na Jamal Soud.
Kutoka Mbeya, Prisons ilinusurika kipigo baada ya kuchomoa bao jioni ikitoka sare ya 1-1 dhidi ya Mbao kwenye Uwanja wa Sokoine.