Simba yatisha, Yanga yaangukia pua

Muktasari:

  • Ligi hiyo inayoendelea ikihusisha timu 16 za vijana kutoka timu 16 za Ligi Kuu imefika hatua hiyo baada ya kumalizika kwa mechi za makundi ambapo yalikuwepo  mawili kila kundi likiwa na timu nane.

TIMU nane za vijana kutoka klabu zinazoshiriki Ligi Kuu zimetinga hatua ya nane bora ya mashindano ya vikosi vya vijana wasiozidi umri wa miaka 20 huku Yanga na bingwa mtetezi, Mtibwa Sugar zikiangukia pua.

Ligi hiyo inayoendelea ikihusisha timu 16 za vijana kutoka timu 16 za Ligi Kuu imefika hatua hiyo baada ya kumalizika kwa mechi za makundi ambapo yalikuwepo  mawili kila kundi likiwa na timu nane.

Azam FC, Coastal Union, Ihefu na Simba zimetinga kutokea kundi A na kuzigaragaza Tanzania Prisons, Yanga, Namungo na KMC zikiaga mashindano.

Kwa upande wa kundi B, zimefuzu timu za Dodoma Jiji, JKT Tanzania, Geita Gold na Kagera Sugar huku Mashujaa, Singida Fountain Gate, Mtibwa Sugar na Tabora United zikiondoshwa.

Mabingwa watetezi waliotwaa taji hilo katika misimu mitano iliyopita mfululizo, Mtibwa wameaga mashindano hayo baada ya kupokwa alama 15 kikanuni kwa kushindwa kufika kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania uliopangwa kupigwa Machi 19.

Kabla ya kupokwa alama hizo 15, Mtibwa ilikuwa na alama 23 ambazo tayari ilikuwa imekata tiketi ya kufuzu nane bora kutoka kundi B, lakini imeshindikana na Geita iliyomaliza na alama 32, sambamba na Kagera iliyokuwa na pointi 21. Mashindano hayo yatapangiwa ratiba.