Mandonga: Ndege ilipotikisika ilitaka kunitoa roho (2)

Muktasari:

Yule muhudumu aliendelea kusema kutokana na hali ya hewa ndege nyingi kutoka mataifa ya mbali zimeshindwa kutua. Baada ya hapo nilisikia ndege ikionyesha mtikisiko kama inadondoka, watu wote kwenye ndege walinyamaza kimya, kilichotokea ikawa kila mtu yupo na Mungu wake.

BONDIA Mandonga ambaye jina lake halisi ni Karim Said, amefanya mahojiano maalum na Mwanaspoti na baada ya jana kueleza mambo mengi kuanzia ajira yake ya zamani ya kupiga debe hadi sasa akiwa bondia maarufu, leo tuendelee naye katika sehemu ya pili ya mahojiano hayo:

SWALI: Kukosa mchezo wa ngumi pengine ulitamani kuwa nani?

JIBU: Nashukuru Mungu kuwa nafasi kubwa inayokufikia ndiyo unayoipokea, binafsi sijawahi kutamani namshukuru Mungu, ujue sisi binadamu Mungu ametuumba mioyo yetu na utofauti wa matamanio.

Kuna mwingine anatamani awe kama mtu fulani na Mungu anaweza kukusaidia ukawa kama huyo mtu lakini je, tabia zake unaweza kuzibeba kama huyo mtu kwa hiyo zinakuwa ni picha za uongo.

Sasa kutamani vitu vingi siyo vizuri, utamani kitu kinachoweza kukufikia, ukawa nacho, kisichokufikia ukakiacha.

Ukiangalia kama mimi nilitamani kupanda ndege ila sikuitamani ndege, nilitamani Mungu akinipangia siku yoyote nipande ndege, siku ilipofikia Mungu akajalia nikapanda kwenda sehemu za watu.

Nilitamani kwenda kupigana taifa jingine nje ya Tanzania, nikaenda Kenya kupigana.

SWALI: Mara ya kwanza kupanda ndege ulijisikiaje?

JIBU: Ilikuwa ni kitu ambacho nimependa kukiona ila leo nabahatika kwenda kukipanda, nilijisikia furaha kubwa, unajua kitu chochote hujakipangilia na unakiona kwa macho halafu inatokea kinakufikia, unakuwa na furaha kubwa mno.

Kwanza mimi nilikuwa siamini kama kwenye ndege kuna watu hicho cha kwanza, cha pili kama kuna watu huwa wanapandia wapi lakini Mungu alivyonisaidia nikaenda kuona watu wanapopandia yaani uwanja wa ndege na mlango wa kupandia.

Niliona siti za kukaa na mule ndani kuna huduma nyingi zikiwemo vinywaji, keki, korosho na huduma nyingine.

SWALI:  Safari yako ya kwanza kupanda ndege ulikuwa unaenda wapi?

JIBU: Safari ya kwanza nilipanda ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma, nilienda kupigana na mwanajeshi mmoja anaitwa Soti Mdudu na Mungu alinijalia nilishuka kwenye ndege na ufalme wangu, nikampiga raundi ya nne.

Safari ya pili kupanda ndege, nilienda Kenya na nilivyorudi nikapanda tena kwenda Bukoba na nilivyotoka huko nikaenda tena Kenya nilivyorudi nikaitwa tena Kenya.

Nilienda kupigana na bondia wa Uganda (Kenneth Lukyamuzi), mimi ni bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, ubingwa nilishinda Kenya, nilivyorudi nikaenda Bukoba na kabla sijapoa baada ya kutoka Bukoba nikaenda Mwanza na ndiyo nilipigwa na Mganda, Moses Golola.

Golola alinipiga raundi ya tatu ila namshukuru Mungu usafiri wa ndege naujua mazuri yake na mabaya yake, ndege siyo nzuri sana moja kwa moja.

Ndege ina utofauti wake mkubwa mno, mwanzo ilipokua inaanza kuruka nilikuwa nasikia utumbo unashuka na inaposhuka nilikuwa nasikia utumbo unashuka lakini siyo hiyo tu, usiombe ndege ikapata msukosuko.

Mungu alinijalia safari moja ya Kenya nilikuwa na promota Meja Seleman Semunyu kwenda kupigana na Mganda, hiyo tuliona misukosuko hatari.

Unajua ndege ilipotea sana juu katika anga basi mhudumu wa kwenye ndege akatutangazia tupo katika anga la juu sana akitaja nyuzi huku akisisitiza tunakaribia kuingia Nairobi.

Lakini yule muhudumu katika taarifa yake aliendelea kusema lakini kutokana na hali ya hewa  ndege nyingi kutoka mataifa ya mbali zimeshindwa kutua.

Baada ya hapo nilisikia ndege ikionyesha mtikisiko kama inadondoka, watu wote kwenye ndege walinyamaza kimya, kilichotokea ikawa kila mtu yupo na Mungu wake.

Lakini mwisho wa yote ilivyofika wakati wa kutua, ikagoma na yule muhudumu akatutangazia hatuwezi tena kushuka kwenye Uwanja wa Ndege wa Nairobi kwa sababu hali ya hewa imechafuka na uwanja umechafuka hivyo tunarudi Arusha.

“Ndege ikageuza kuanza kurudi Arusha ila kufika kati tukakutana na misukosuko mengine kila mmoja nilimsikia akimtaja Mungu mpaka Wazungu nao walikuwa wakimtaja Mungu ila mwisho wa hapo ndege iligeuza na kurudi Kenya kwa kuizunguka ndiyo tukaweza kutua,” anasema Mandonga.

SWALI:  Francis Cheka na Twaha Kiduku umewasapoti mara nyingi kama shabiki wao kwenye ngumi, nani alikuvutia hadi ukaamua kuingia mwenyewe?

JIBU: Mtu ambaye amenifanya nipende au kuwa bondia ni Mike Tyson, amenishawishi kwa muda mrefu.

Lakini kwa hapa nyumbani watu ambao nilikuwa nawapenda na kunipa ushawishi wa kuwasapoti alikuwa ni Francis Cheka kipindi katoka kwao Msumbiji kuja Morogoro sisi ndiyo tulikuwa watu wake wa karibu.

Nilikuwa shabiki mkubwa sana wa Cheka hata kama mwenyewe akisikia huko alipo hawezi akakataa, nilikuwa naenda kutafuta riziki yangu stendi nikimaliza naenda gym na mchango wangu kwake yeye afanye vizuri kwenye mapambano yake.

Nilikuwa nampenda sana Cheka lakini baadaye akaja mdogo wangu Twaha Kiduku na kabla alikuwa akija kuangalia mazoezi ila ilifika kipindi akaja kujiunga na hata baadhi ya mapambano yake nilikuwa nampandisha kwa kumbeba mabegani kupanda ulingoni mwenyewe.

Sasa hivi mabondia ambao nawapenda na kuwashabikia ni Twaha Kiduku, Seleman Kidunda, Mfaume Mfaume, Idd Pialali na wengine waliobakia ila hao wanne nawapenda sana.

SWALI: Ushapigana na mabondia wa nje na ndani ya Tanzania, kwa sasa unatamani upigane na nani kutoka nje?

JIBU: Sijawahi kuchagua bondia, Mandonga ‘Mtu Kazi’ siku zote hachagui kazi, bondia yeyote akiwa wa Tanzania ukiwaondoa hao niliokutajia, napita naye kama kipanga na yeyote kutoka nje ukiwandoa Tyson na Floyd Mayweather napita nao.

SWALI:  Nilisikia unataka kupigana na Harmonize, imefikia wapi?

JIBU: Harmonize ametangaza vita na alipotangaza vita katika mchezo wa ngumi maana yeye vita yake ni ya muziki na sisi mabondia manguli tupo na yeye ametangaza na anataka kuona burudani ya mchezo wa ngumi, mimi ndiyo kazi yangu inayosababisha niishi mjini.

Nimemwambia usipate tabu akitaka pambano muda na wakati wowote milango yangu mimi ipo wazi maana yeye anajiita Tembo ila siyo Tembo, tunamtupa kule anakuwa Sungura na kama anajiita jeshi, lakini hana kofia, basi yeye ni mgambo tu.

Kipigo chake yeye kinamuhusu, muda wowote wakati wowote na wala sijafundishwa na mtu limetoka moyoni kwangu, Harmonize ajipange na ajue watu wapo tayari muda wowote.

SWALI:  Siyo kwamba unafuata upepo wake wa kuwa ni msanii mwenye jina kubwa?

JIBU: Sidhani kama ana jina kubwa kama Mandonga ‘Mtu Kazi’ Icon ya Tanzania, tukipita mtaani mimi na yeye, atajulikana na watu watano, mimi wanane ila kwa kuwa ametaka kutrendi kupitia ngumi basi aje.

SWALI:  Inakuchukua muda gani kurudi kwenye hali ya kawaida unapopigwa ngumi kali?

JIBU: Kiukweli siyo dakika nyingi, nalewa dakika chache narudi kwenye fomula kwa sababu ni mchezo wa ngumi maana wanasema binadamu akishakupatia amekupatia.

Wanasema kama ukipoteza muelekeo umepoteza maana mchezo wa ngumi ni hatari kwa hiyo unapotokea kupoteza mweleko na kurudi kwenye ‘network’ yako siyo akili inavurugika ila kuna kitu kinakuwa kinakuchukua kwa muda kisha unakaa sawa.

SWALI: Hivi unapopigwa ngumi ya kidevu ndiyo unavurugika?

JIBU: Katika dunia hakuna binadamu mwenye kichwa ambacho kinachuma au gadi ndiyo maana wakasema Mandonga wewe ni kichwa cha bata ila niliwaambia kama cha bata basi leo siyo cha bata kimekuwa cha kuku, kinakwepa hata jiwe.

Nadhani kazi hiyo alikutana nayo mtu mmoja wakuitwa Said Mbelwa hata ukirusha jiwe kichwa kinakwepa.

SWALI:  Mipango yako inasimamia wapi kwa sasa?

JIBU: Binafsi kwa sasa nawasikiliza mapromota wanitafutie bondia yeyote nitacheza naye na hapa najiandaa maana hata Shaban Kaoneka tayari kuna wadhamini wameanza kujitokeza kuweka pambano la marudiano.

Sasa kazi hii inaweza kupigwa muda wowote, wakinisainisha naweza kumfuata Makongorosi, Chunya kwa sababu Kaoneka amekimbilia kwenye madini.

Sasa nitakachokuja kumuonyesha ni kwamba nitamfuata huko Chunya kwenye madini kumuonyesha ‘action’ nitamshushia kipigo cha kwenye madini, sichagui bondia yeyote atakayekuwa tayari nitapanda naye.

SWALI:  Kwa nini unaonekana mdogo kuliko wao?

JIBU: Unajua kila siku zinavyokwenda huwa nashusha umri wangu, sasa hivi mimi ni Serengeti Boy yaani nina miaka 15.

Mungu kaniwekea baraka ya mtu pekee kupunguza umri kutoka miaka 45, nikashuka mpaka kwenye miaka 28, sasa hivi nimeshuka nakuwa Serengeti Boy ambapo nitaanza kukua kuanzia miaka 16 kwenda juu, mimi ni mtu pekee niliyepata bahati hiyo. Mandonga ni Serengeti Boy.

SWALI:  Ushawahi kupigwa na kutamani kuacha ngumi?

JIBU: Aaah! Haijawahi kutokea kwa sababu Mandonga ndiyo mtu wa kwanza kuipenda ngumi, nadhani mwenyewe uliona nilipigwa na Magambo KO raundi ya kwanza, watu wakajua sitoweza kurudi kwenye ngumi ila ndiyo kwanza nilinoga.

Nilikuja kwenye pambano la pili Songea, nikapigwa na Shaban Kaoneka wakajua Mandonga ngumi ndiyo basi tena ila ndiyo ikawa kama nimewekewa biriani kwenye ngumi. Ngumi kwa Mandonga kuacha labda niwe na miaka 73.

SWALI:  Una familia ya watoto wa ngapi?

JIBU: Namshukuru Mungu, nina familia ya watoto sita, wa kiume watatu na wa kike watatu hao ndiyo wapo katika himaya yangu.

SWALI:  Kama siyo mchezo wa ngumi, ulikuwa na ndoto gani?

JIBU: Binafsi sijawahi kuwa na ndoto ya kusema Mungu anifanye niwe mtu fulani ila nashukuru kila ninaposimama nakuwa namba moja.

Nilisimama kwenye kupiga debe, mpiga debe maarufu nilikuwa mimi, mpaka nimeondoka hakuna mpiga debe aliyenifikia, baadaye nilingia kwenye mfumo wa kupiga tofali na nikawa namba moja.

Unajua katika matanuri yangu likiwa dogo basi lina milango mitatu, nilikuwa napiga hadi tanuri la milango sita mpaka nane kwa tofali 30,000 hadi 40,000, sijawahi kusimamisha tanuri dogo.

Nikaingia kwenye soka na nikawa shabiki namba moja na nikipangwa ndani kama mchezaji nacheza yaani huwezi kuamini kama mchezaji unaweza kusema ni Pacome au Mayele.

Lakini nikahamia kwenye muziki nikawa densa namba moja Wilaya ya Kilosa na Mkoa wa Morogoro nikiwa namba tatu wakati huo naitwa Super Kali.

Baada ya hapo nikaingia kwenye ngumi kama shabiki namba moja ambaye nachangisha pesa za watu, nakodi basi naleta mashabiki wote wa kidedea katika mapambano ya Cheka Dar es Salaam.

Ukiachana na hilo ndiyo ndiyo shabiki namba moja kumshabikia Twaha Kiduku akiwa mdogo wetu tumemfundisha ngumi sisi wenyewe hadi ‘sparing’ nimempa.

Baada ya hapo nikaamua kuingia mwenyewe kama bondia na nimekuwa bondia namba moja ninayeuburudisha mchezo wa ngumi.

SWALI:  Umesema wewe ni shabiki wa Yanga, mchezaji gani unayemkubali?

JIBU: Naipenda Yanga kwa Tanzania, nina vitu ninavyopenda na siwezi kupinduliwa, kwanza nakipenda chama tawala CCM na katika mpira ndiyo hiyo Yanga.

Naipenda Yanga kuanzia kwenye uongozi na kuna baadhi ya wachezaji wa Yanga nawapenda, wapo ambao wameondoka.

Nilimpenda mdogo wangu Fiston Mayele, Simon Msuva, nikaja kumpenda Feisal Salum ‘Fei Toto’, halafu kuna mtu mmoja anaitwa Tuisila Kisinda.

Nilikuwa nawapenda kwa sababu ya burudani zao wanazoonyesha kwa Wananchi.

SWALI: Umemtaja sana Mayele kwa nini?

JIBU:Unajua ukienda kwenye ngumi kwa burudani unamkuta Mandonga na kwenye soka ni yeye alikuwa anapambana na akifunga basi atatetema kwa ile staili yake ni mtu niliyekuwa namuelewa sana.

SWALI: Sasa hivi unampenda mchezaji gani?

JIBU: Tanzania yote wamepata habari yake na habari ya Tanzania ni Pacome Zouzoua yaani hilo siyo la kuuliza.

SWALI:  Kwa nini Pacome na siyo Aziz Ki?

JIBU: Unajua siyo yeye anayecheza peke yake ila moyo wangu umetokea kumpenda yeye zaidi na zaidi. Lakini wapo wengine wanauliza Yanga unaipendea nini.

Naipenda siyo sababu ya wachezaji peke ila nawapenda hadi viongozi wake kama Injinia Hersi na mdogo wangu aliyeingia sasa hivi Ally Kamwe kumpokea msemaji mkuu Haji Manara.

Ally Kamwe ndiyo meneja wangu wa kwanza katika mchezo wa ngumi, ndiyo aliyenileta mjini na kunionyesha mwanga ni yeye.

SWALI: Nje ya ngumi Mandonga ni mtu wa aina gani?

JIBU: Mimi ni baba wa familia, nikitoka nje ya ngumi nakuwa na familia yangu nyumbani, mke wangu ambaye alikuwa anaitwa Catherine Andrea, nimembadilisha dini na sasa anaitwa Nuru Andrea.

Kwa upande wa wanagu, wa kwanza ni Khalid halafu kuna Idrisa na Halima, wengine ni Jasmini, Sharifu na Sharifa.

SWALI: Katika watoto wako sita kuna ambaye amefuata nyayo zako?

JIBU: Hawa wakubwa hawajafuata nyayo zangu ila kuna mwamba moja yeye anaitwa Sharifu huyo ndiyo Mandonga ‘Mtu Kazi’, sasa anasoma darasa la tatu, hafai kabisa.

Yeye kwanza ana hasira vibaya na ameshasema anataka aje alipize kisasi kwa baba yake kupigwa ila nimemuambia muda ambao yeye anataka kulipiza kisasi hao watu watakuwa wameshakuwa wazee au Mungu amewachukua.

Lakini nimemwambia akitaka kufanya hivyo labda kwa watoto wao kwa kuwa watakuwa wa rika lake na naamini watakuja kukutana hapo baadaye ili alipize kisasi kwa watoto zao.

Namkubali kupita uwezo hii misemo yangu ya kutaja ngumi kama hii nitaita ndoige na yeye anazo zake na amekuwa akiniambia ana vitu vya kigeni ipo siku muda wake ukifika ataniambia.

SWALI: Kitu gani kingine ambacho mashabiki wako unatamani wakisikie?

JIBU: Napenda mashabiki wangu wasikie misemo yangu mipya nitakayokuwa naiachia maana siyo muda mrefu nitarejea ulingoni yaani kama sijapata mechi ya kucheza hapa ndani basi naweza kwenda kucheza Misri.

Nitakuwa na pambano la kwenda kucheza Misri na Mungu akipenda kuna pambano nitaenda kucheza Uingereza, nikishasaini mikataba nitawatangazia na msemo ambao nitaachia.

Mwisho