Simba yashusha kiboko ya Kamusoko

Muktasari:
- Mabosi hao wa Simba kupitia Rais wao, Evans Aveva na Kamati yake ya Usajili chini ya Mwenyekiti, Zakaria Hanspoppe walikuna vichwa kabla ya kufanya maamuzi ambayo yatawafanya Wanamsimbazi kutabasamu kwa furaha.
YANGA imekuwa ikiwatambia watani zao mitaani kwa sababu ya mtu mmoja tu, Thabani Kamusoko ‘Rasta’ anayepiga soka la kufa mtu pale kati akigawa mapande makali kwa staili ya Kampa Kampa tena...!
Soka la Kamusoko akishirikiana na Haruna Niyonzima liliwarahishia kazi mastraika wa Yanga kiasi cha kuwavuruga Vijana wa Msimbazi ambao msimu uliopita wapigiwa nje ndani katika Ligi Kuu Bara, jambo lililowatikisa mabosi wa timu hiyo.
Mabosi hao wa Simba kupitia Rais wao, Evans Aveva na Kamati yake ya Usajili chini ya Mwenyekiti, Zakaria Hanspoppe walikuna vichwa kabla ya kufanya maamuzi ambayo yatawafanya Wanamsimbazi kutabasamu kwa furaha.
Aveva na wenzake wamefanikiwa kupata dawa ya kumaliza ubabe wa Kamusoko kwa kuamua kushusha bonge la kiungo mshambuliaji matata kutoka DR Congo, huku wakiwa mbioni kumleta mrithi wa Justice Majabvi aliyeikacha timu hiyo.
Kiboko huyo wa Kamusoko ni Musa Ndusha akitokea klabu ya FC Renaissance du Congo ya DR Congo, ambaye jana Alhamisi katika mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, jijini Dar es Salaam ni kama alikuwa akimharakisha Kocha Joseph Omog kumsainisha fasta.
Kiungo huyo alionyesha mpira mwingi wa kiufundi, akionyesha ni mjanja mjanja sana uwanjani yaani alikuwa akitema mate kulia na kufukia kushoto na kama kweli mabosi wa Msimbazi watamsainisha basi watakuwa wamemaliza kazi mapema ya kumshika Kamusoko ambaye amekuwa akitamba tangu atue nchini akitokea kwao Zimbabwe.
Katika mazoezi ya jana ambayo yalisimamiwa vilivyo na Kocha Omog pia kulikuwa na wakali wengine wawili wa kigeni, straika wa zamani wa Asante Kotoko ya Ghana na Club Africa ya Ivory Coast, Fredrick Blagnon kutoka Ivory Coast pamoja na beki Janvier Bokungu kutoka DR Congo.
Mazoezi yalivyokuwa
Kikosi hicho ambacho kilifanya mazoezi kwa takriban saa mbili na nusu kuanzia saa 2:30 hadi saa 5:00, ambapo walianza kufanya mazoezi ya viungo, mbio pamoja na kucheza mechi ya wenyewe kwa wenyewe.
Mazoezi ambayo yalichukua muda mwingi ni mbio na yalichukua zaidi ya saa nzima ambapo wachezaji waligawanywa katika makundi mawili, moja likiwa na Omog na lingine la pili likiwa na msaidizi wake, Jackson Mayanja raia wa Uganda.
Ambapo wachezaji walikimbia katika eneo la uwanjani pamoja na sehemu nyingine ndani ya eneo hilo la chuo na walienda hadi ilipo gym ya uwanjani hapo.
Katika mechi ya wenyewe kwa wenyewe ndipo, Ndusha alipoonyesha alivyo mkali katika kulichezea gozi la ng’ombe, akifanya atakavyo kiasi cha kumfanya Kocha Omog kutabasamu.
Wachezaji walioshiriki mazoezi hayo ukiondoa wageni hao wapya ni pamoja na makipa Vincent Angban, Peter Manyika na Richard Dennis. Wengine ni Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’, Said Ndemla, Novat Lufunga, Peter Mwalyanzi, Mussa Hassan Mgosi, Mwinyi Kazimoto, Awadh Juma, Yasin Mudhamiru na Mohammed Ibrahim.
Wachezaji wa kikosi cha Vijana U20 walikuwapo ni pamoja na Kelvin Longbety, Moses Chitandu, Mohammed Mussa, Said Khamis na Kelvin Mkude.
Benchi laimarishwa
Wakati mazoezi yakiendelea yupo jamaa mmoja alikuwa amekaa sambamba na Makamu wa Rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na Collins Frisch ambaye baadaye alitambulishwa kwa wachezaji kama mtu wa Benchi la Ufundi kutoka nchini Zimbabwe.
Awali ilidhaniwa kuwa jamaa huyo ndiye kiungo mkabaji ambaye ametajwa kuwindwa na Simba ili kurithi nafasi ya Justice Majabvi anayedaiwa kutimkia Austria lakini mmoja wa viongozi wa Simba alilidokeza Mwanaspoti kuwa: “Huyu ni jamaa wa benchi la ufundi, ndio maana umeona kaondoka na Kocha Omog.”
Katika hatua nyingine Kocha Omog na Meneja Abbas Ally waliliambia Mwanaspoti kuwa, kambi ya mazoezi rasmi kwa msimu mpya itaanza Jumapili mjini Morogoro.