Simba SC yatakiwa kuomba radhi ikidaiwa kudhalilisha wenye ualbino

Muktasari:

  • TAS na LHRC wamewaitaka klabu Simba kutoka hadharani na kuomba radhi umma na watu wenye Ualbino kwa kitendo cha klumpandisha jukwaani mtu mwenye ualbino akiwa amevishwa taulo ya kitoto.

Dar es Salaam. Chama cha watu wenye Ualbino Tanzania (TAS) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wameitaka klabu ya Simba kuomba radhi kwa tukio waliloita la udhalilishaji.

Tukio hilo lilitokea Agosti 6, 2023 kwenye sherehe ya tamasha la siku ya Simba yaliyofanyika uwanja wa Taifa wa Benjamini Mkapa jijini hapa kwa kumpandisha mtu mwenye ulemavu wa ngozi akiwa amevishwa taulo ya watoto (baby diaper).

Msemaji wa Simba Ahmed Ally alipoulizwa kwa simu leo, amesema wamesikia na wapo tayari kufanya hivyo.

“Wamesema tuombe radhi? Basi sawa. Kwa sasa tuko busy na mechi ya kesho, akili yetu yote ipo kwa kwa ajili ya kesho. Haya mambo mengine tukianza kujibu tutavuruga utaratibu. Nitamuuliza CEO tuone tunafanya nini,” amesema.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 9, 2023 jijini Dar es Salaam mwenyekiti wa TAS, Godson Mollel amesema tukio hilo ni la pili kwa Simba kulifanya ambalo la kwanza lilikuwa Agosti 8, 2022 waliingia na jeneza ambalo lilimbeba mtu mwenye ualbino.

Amesema vitendo hivyo vinawatweza utu wa watu wenye ualbino nchini na kupelekea kuwepo kwa mijadala mingi katika jamii ikiwemo mitandaoni inaonyesha dhihaka kwa watu hao kinyume na haki za binadamu.

Mollel amesema kwa miaka mingi kumekuwa na jitihada kubwa za utetezi wa watu wenye ualbino nchini kutokana na historia ya madhila yaliyopelekea watu hao kupoteza maisha,pamoja na idadi kubwa ya wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyapaa.

"Tunasisitiza utani wa jadi uliopo wa Simba na Yanga hauhalalishi vitendo vya kutweza utu wa mtu kwa sababu yoyote ile iwe kwa kukusudia ama kwa kutokukusudia," amesema Mollel.

Pia, amesema jamii nyingi watu wenye ualbino wamekuwa wakihusishwa na mila na tamaduni mbaya zinazotweza utu wao, hivyo kuendelea kwa vitendo hivyo ni kudididmiza juhudi za serikali, Mashirika watetezi na wadau binafsi za kuelimisha jamii kuhusu ualbino.

Amesema vitendo vya namna hii vinaporuhusiwa kufanywa hususani na taasisi kubwa ya Simba yenye ushawishi kwa jamii inarudisha nyuma kwa kiasi kikubwa jitihada zote zinazofanywa za katika kuhamasisha taswira chanya za watu wenye ualbino.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Anna Henga ametoa rai kwa taasisi zote zenye ushawishi katika jamii hususani timu kubwa za mpira wa miguu kuepukana na vitendo vyenye sura ya udhalilishaji na badala yake wajikite katika kuhamasisha heshima na utu.

Henga amewataka watu wenye ualbino kutochukulia vitendo vya aina hiyo kwa wepesi na badala yake kuvikemea vikali kwa maana na wao ni binadamu kama wengine wenye haki ya kutodharirishwa na kuheshimiwa na utu wao.

Pia amewataka uongozi wa Simba kuomba radhi kwa watu wenye ualbino na umma kwa vitendo vya kutweza utu wao,na kuiomba Serikali pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kusimamia jambo hilo.