Simba yashinda, Yanga ikipasuka
LIGI Kuu ya vijana chini ya miaka 20, imeendelea kupigwa katika viwanja mbali mbali ambapo wikiendi hii ilishuhudiwa Simba ikionja ushindi wake wa kwanza huku Yanga ikipoteza mechi ya kwanza.
Yanga ilijikuta ikichezea kichapo cha mabao 2-0, kutoka kwa Azam ikiwa ni mechi yake ya kwanza kupoteza kwani mechi mbili za mwanzo ilitoa sare huku Simba ikipata ushindi wa kwanza kwa kuifunga Ihefu 1-0, baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo.
Ushindi ilioupata Dodoma Jiji wa bao 1-0 mbele ya Kagera umeifanya kuwa timu pekee iliyoshinda mechi zote nne hadi sasa ikiongoza kundi B na pointi12, huku Azam ikiongoza kundi A na pointi tisa.
Katika ligi hiyo inayochezwa kwa makundi mawili, inahusisha timu 16 za vijana wa U-20, kutoka katika timu za Ligi Kuu, ikichezwa kwa makundi mawili ambapo kundi A linaongozwa na Azam Coastal Union, Tanzania Prisons, Namungo, Simba, Ihefu, KMC huku Yanga ikibuluza mkia.
Kundi B linaongozwa na Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar, Singida Big Stars, JKT Tanzania, Geita Gold, Mashujaa, Tabora United na Kagera Sugar iliyo mkiani na Ligi itanendelea wiki hii.