Simba yapewa ratiba ya kibabe

BAADA ya ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Dodoma Jiji FC juzi, Simba inakabiliwa na siku 22 za machozi jasho na damu ambazo zimeshikilia hatima yake katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Ndani ya kipindi hicho, Simba itacheza mechi tano ngumu za Ligi Kuuu na Ligi ya mabingwa Afrika ambazo kama itachanga vyema karata zake, itakuwa na nafasi kubwa ya kutamba katika mashindano hayo mawili muhimu kwake.
Lakini kinyume chake, kama Simba itashindwa kujitutumua na kupata matokeo mazuri katika mechi hizo, inaweza kuweka rehani matumaini yake ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kutokana na aina ya timu watakabiliana nazo na ufinyu wa muda wa kupumzika na kujitayarisha kutoka mechi moja hadi nyingine.
Simba ndani ya muda huo itacheza mechi tatu za Ligi Kuu dhidi ya Azam, Yanga na Ruvu Shooting lakini pia itakuwa na mechi mbili za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita na Al Ahly lakini pia italazimika kuwa wastani wa siku nne za mapumziko na maandalizi kutoka mechi moja hadi nyingine.
Shughuli kwa Simba itaanzia kesho Jumapili, Februari 7 wakati watakapoialika Azam FC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiwa ni miongoni mwa mechi zake za viporo kama ule wa juzi dhidi ya Dodoma Jiji FC.
Ushindi dhidi ya Azam utaifanya Simba iwe nyuma ya Yanga inayoongoza msimamo wa ligi kwa utofauti wa pointi tatu huku ikibakiwa na mchezo mmoja wa kiporo dhidi ya Namungo FC lakini kama itapoteza au kutoka sare, utaipunguza kasi katika mbio za kuwania ubingwa dhidi ya Yanga. Ifahamike kwamba kama Simba itashinda mechi zake mbili za viporo dhidi ya Azam na Namungo, itakwea kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kunufaika na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa wa Simba ni mabao 33 wakati ule wa Yanga ni mabao 22 hadi sasa.
Baada ya kuikabili Azam, Simba itakuwa na siku tano za kusafiri na kucheza mechi yake ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita ya DR Congo utakaochezwa jijini Kinshasa, Februari 12
Ikishamalizana na AS Vita ugenini, Simba itarejea na kukutana na mechi ngumu ya Ligi Kuu dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga ambao utachezwa Februari 20 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.
Ushindi dhidi ya Yanga maana yake utawaweka Simba katika nafasi nzuri ya kuwapiku watani wao kileleni mwa msimamo lakini kama wakipoteza au kutoka sare, maana yake wataiweka Yanga katika fursa nzuri ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Siku tatu baadaye, Simba itaikaribisha Al Ahly katika mechi ya pili ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu utakaochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Baada ya mchezo dhidi ya Al Ahly, Simba itakuwa na mechi ya kisasi katika Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting itakayochezwa Februari 28. Ikumbukwe kwamba, Ruvu Shooting waliifunga Simba kwa bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu.
Kocha wa Simba, Didier Gomez Da Rosa alisema wanakabiliwa na ratiba ngumu lakini watahakikisha wanafanya vyema.
“Ni ratiba ngumu lakini tuko tayari kukabiliana nayo na kuhakikisha tunafanya vizuri. Malengo yetu ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo ili yatimie lazima tufanye vizuri katika mechi nzuri.
Jambo la kutia moyo ni kwamba tuna wachezaji wazuri ambao wanaweza kuhimili ratiba hiyo iliyo mbele yetu,” alisema Gomez.
Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema Simba inaweza kukabiliana na ratiba hiyo kama itajiandaa vyema.
“Kinachohitajika ni maandalizi tu kwani mechi zote hizo zina umuhimu. Naamini benchi la ufundi la Simba na viongozi wake watajipanga vyema ili iweze kufanya vizuri,” alisema Pawasa.