Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndio hivyo…. Na badooo

MSIMBAZI viporo havichachi. Ndio, Simba ikiwa ugenini jijini hapa ilikula kiporo cha kwanza cha Ligi Kuu Bara kiulaini kwa kuifumua Dodoma Jiji mabao 2-1, huku winga Bernard Morrison ‘BM3’ akiendelea kuwakera mashabiki wa upande wa pili kwa kuhusika na mabao yote.

Mghana huyo alianzishwa kwenye mchezo huo na hakumuangusha Kocha Didier Gomes aliyeiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu kwa kuasisti bao kipindi kwa kwanza na kisha kufunga la ushindi lililowapa Simba ushindi kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Ushindi huo ulipatikana kwa mbinde kutokana na Dodoma kuonyesha upinzani muda wote wa dakika 90 licha ya kuangushwa na uzoefu kulinganisha na wapinzani wao, umeifanya Simba kufikisha pointi 38 baada ya mechi 16 na kupunguza pengo la pointi kati yao na Yanga kubakia sita.

Katika pambano hilo lililochezeshwa vyema na mwamuzi Emmanuel Mwandembwa, Kocha Gomes alimuanzisha Morrison sambamba na Meddie Kagere, Clatous Chama na Luis Miquissone eneo la mbele na kuwakimbiza wenyeji wao, ingawa Dodoma walijitahidi kuwazuia wasiwadhuru.

Hata hivyo, katika dakika ya 30 kosa la mabeki wa Dodoma kujipanga liliwapa faida Simba kuandika bao la lililowekwa kimiani na Meddie Kagere kwa kichwa akimalizia krosi ya BM3 mpita uliotokana na kona fupi iliyopigwa na Chama dakika 30.

Kuingia kwa bao hilo kulimfanya Kocha wa Dodoma, Mbwana Makatta kumtoa Steven Mganga na kumuingiza Cleophas Mkandala, mabadiliko yaliyozaa matunda kwani dakika chache kiungo huyo wa zamani wa Tanzania Prisons kuwepo uwanjani aliisawazishia bao timu yake.

Mkandala alifunga dakika ya 35 kwa kichwa akimalizia kona iliyopigwa Dickson Ambundo na mfungaji huyo kuruka mbele ya mabeki wa Simba na kumtungua Aishi Manula, likiwa bao la sita kwa watetezi hao kufungwa Ligi Kuu ya msimu huu.

Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko na kipindi cha pili, Gomes alimtoa Luis na kumuingiza Perfect Chikwende na kuiongezea timu yake nguvu kwani dakika ya 65 alipokea pasi murua ya Bwalya na kumpenyezea Morrison aliyefumua shuti kali kuandika bao la pili.

Bao hilo liliwaamsha mashabiki wa Simba ambao walikuwa wamepoa kwa namna Dodoma walivyokuwa wakilisakama lango lao na pia lilikuwa la pili kwa Morrison katika Ligi Kuu baada ya lile alilowatungua Coastal Union Novemba 21 mwaka, jana jijini Arusha.

Timu zote zilifanya mabadiliko mengine, Dodoma ikimtoa Mcha Khamis ‘Vialli’ na kumuingiza Peter Mapunda na baadaye Jamal Mtegeta kumpisha Enriq Nkosi, huku Simba ikiwatoa Morrison na kumuingiza Mzamiru Yassin kisha kumtoa Bwalya ili aingie Ibrahim Ajibu. Mabadiliko ambayo hayakubadilisha matokeo yaliyoiacha Dodoma ikisalia nafasi ya 10 na alama 22.

Kocha Gomes alifurahi kupata ushindi katika mechi yake ya kwanza ya ligi akiwa na Simba, lakini alisema mchezo ulikuwa mgumu na wenyeji walionyesha ushindani mkubwa na anajipanga kwa mechi ya pili ya kiporo Jumapili dhidi ya Azam FC.

Alisema anajua mechi dhidi ya Azam itakuwa ngumu, lakini kiu yake ni kupata matokeo mazuri kabla ya kuanza kazi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa Kundi A na wataanzia ugenini dhidi ya As Vita ya DR Congo.

Naye Kocha wa Dodoma, Makatta alisema vijana wake waliangushwa na bahati pamoja na uzoefu na kuwasifu kwa kucheza vizuri kwenye mchezo huo licha ya kupoteza nyumbani.

Vikosi vilivyocheza

DODOMA JIJI: Kalambo, Wawa, Ngalema, Samson, Bakary, Hoza, Mtegeta/Nkosy, Sylvester/Mkandala, Danga, Mcha/Mapunda na Ambundo

SIMBA: Manula, Kapombe, Tshabalala, Kennedy, Wawa, Lwanga, Chama, Bwalya/Ajibu, Kagere, Morrison/Mzamiru, Luis/Chikwende

IMEANDIKWA NA JALILU MATEREKA na KHATIMU NAHEKA