Prime
Simba, Yanga zaongezewa noti Afrika

KLABU zinazoshiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, zikiwamo Simba na Yanga za Tanzania Bara na Mlandege ya visiwani Zanzibar zimeongezewa neema baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuongeza fedha kwa timu zinazotolewa hatua ya awali.
Simba, Yanga na Mlandege zitaiwakilisha nchi katika Ligi ya Mabingwa, wakati Azam, Singida BS na KMKM zenyewe zitacheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2025-2026 utakaoanza Septemba mara baada ya fainali za michuano ya Kombe la Mabingwa wa Afrika (CHAN) 2024.
Taarifa nzuri kwa klabu zitakazoshiriki Ligi ya Mabingwa ni kwamba kuanzia msimu uliopita ambapo Umoja wa Klabu Afrika (ACA) unaongozwa na Mwenyekiti Injinia Hersi Said uliwasilisha ombi la klabu zinazotolewa awali kupata fedha angalau kifuta chasho zitakazowaondolea uchovu.
CAF imeyafanyia kazi maombi hayo na sasa kuanzia msimu ujao utakaoanza Septemba mwaka huu, shirikisho hilo litoa kiasi cha Dola 50,000 (zaidi ya Sh 132 milioni) kwa klabu zote zinazoishia hatua ya mtoano, ambazo zimekwama kutinga makundi.
Hata hivyo, ACA tena kupitia mkutano wa Kamati ya Utendaji ya CAF ikawasilisha tena maombi ya klabu hizo kuongezewa fedha hizo na ombi hilo kupita.
Mkutano huo ambao umefanyika juzi, jijini Rabat, Morocco, umeziongezea klabu hizo zinazotolewa hatua ya awali kutoka Dola 50,000 na itaongezeka mbele ya safari hadi kufikia Dola 100,000.
Rais wa CAF, Dk Patrice Motsepe wakati wa kutangaza kwa ongezeko hilo ameipongeza ACA kwa kuendelea kuzifanyia kazi changamoto za klabu, huku akithibitisha Shirikisho hilo linaendelea kufanyia kazi mambo mbalimbali kutoka kwa umoja huo ili kuhakikisha soka la Afrika linasonga mbele.
Kabla ya mabadiliko hayo klabu zilizokuwa zikitolewa hatua za awali hazikuwa zinaambulia chochote isipokuwa zikiwa makundi ambapo kwa Ligi ya Mabingwa inayoshika nafasi ya tatu na nne zikitolewa hatua hiyo zilikuwa zikivuna dola 700,000 (zaidi ya Sh 1.9 bilioni) wakati katika Kombe la Shirikisho zilizoshindwa kutinga robo fainali ziliambulia dola 400,000 (zaidi ya Sh 1 bilioni).