SIMBA, YANGA NI SHIIDA!

Muktasari:
Hata hivyo, ukiangalia usajili uliofanywa na timu hizo kwenye safu ya ulinzi, kiungo hata mastraika makocha watalazimika kutumia akili za ziada kupanga vikosi vya kwanza kwani ushindani mkubwa umeonekana mazoezini na kwenye mechi za kirafiki baina ya wachezaji husika.
NI Shiida! AZAM ndiyo klabu tajiri na yenye udhamini mnono zaidi Tanzania Bara. Ina udhamini wa zaidi ya Sh1 bil kwa mwaka, potezea kidogo hiyo ishu. Simba na Yanga zilikuwa zimejificha Zanzibar kujiwinda na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, ukiangalia usajili uliofanywa na timu hizo kwenye safu ya ulinzi, kiungo hata mastraika makocha watalazimika kutumia akili za ziada kupanga vikosi vya kwanza kwani ushindani mkubwa umeonekana mazoezini na kwenye mechi za kirafiki baina ya wachezaji husika.
SIMBA
MNYAMA ana makipa watatu langoni Ivo Mapunda, Hussein Shariff ‘Casillas’ na chipukizi Manyika Peter. Hapa kazi ipo kwa Ivo na Casillas japokuwa mwenye nafasi ya kucheza ni Ivo kutokana na uzoefu na rekodi zake. Kwenye beki ya kulia, ingawa Kocha Patrick Phiri ana imani na Nassor Masoud ‘Chollo’ kutokana na uzoefu wake ukweli ni kwamba anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Adam Miraji na William Lucian ‘Gallas’. Lakini majeruhi yakimwandama kama kipindi cha nyuma atarejea jukwaani.
Beki ya kushoto, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ amekuwa akianzishwa lakini Abdi Banda na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wote wapo vizuri na Baba Ubaya akiharibu tu, wanapasha moto misuli. Phiri amekuwa na imani zaidi na Baba Ubaya.
Joseph Owino ndiye mchezaji pekee mwenye uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza cha Simba akicheza beki ya kati lakini baada ya kuondoka kwa Donald Mosoti atalazimika kucheza ama na Joram Mgeveke au Rajab Isihaka japokuwa Mgeveke ana nafasi kubwa ya kuanza na Owino. Lakini Mwanaspoti linajua kwamba Phiri anafikiria kumjaribu majeruhi Jonas Mkude atakapokuwa fiti asimame na Owino.
Mrundi Pierre Kwizera anacheza kama kiungo ambapo katika mechi zote za kirafiki amekuwa akipangwa katika kikosi cha kwanza hiyo inatokana kwamba mpinzani wake Jonas Mkude yupo nje kwa majeraha na kocha hamjui na vilevile anafikiria kumrudisha nyuma.
Katika winga ya kulia, Amri Kiemba hana mpinzani lakini Phiri anaweza kubadili mawazo na kuwatumia Emmanuel Okwi au Uhuru Seleman kucheza nafasi hiyo inapobidi, pia kiungo Shaaban Kisiga yupo vizuri katika kiungo mshambuliaji japokuwa Said Ndemla naye anaweza kucheza nafasi yake. Chipukizi Ibrahim Ajibu naye anataka nafasi hapa ingawa ameambiwa atulize mzuka asome mchezo.
Mfungaji Bora wa msimu uliopita Amissi Tambwe ndiye chaguo la kwanza la Phiri katika nafasi ya straika lakini ana changamoto kutoka kwa Elius Maguli ambaye ana uwezo wa kupiga mashuti makali tofauti na Tambwe. Mara kadhaa Phiri amekuwa akimtumia Maguli kama mbadala wa Tambwe na amemtangaza kama Supersub mpya Msimbazi.
Kwenye namba kumi nako shughuli ipo kwani yupo Raphael Kiongera na kama sakata la Okwi likiisha kwa mchezaji huyo kuichezea Simba basi kazi atakuwa nayo. Itategemea na ubora wake mazoezini kwani anaweza kuanzishwa Kiongera halafu Okwi akapelekwa namba 11 ambako wapo Haroun Chanongo, Ramadhan Singano na Ibrahim Twaha.
Kama Phiri atatumia mfumo wa 4-4-2 basi Okwi atacheza pembeni, Tambwe na Kiongera watacheza mbele, Kisiga atacheza namba nane na Kiemba atacheza namba saba.
YANGA
Karibu nafasi zote kwenye kikosi cha Yanga zina ushindani, na mchezaji atakayesinzia kidogo tu atajikuta akihesabu vyenga vya Coutinho Jukwaani. Ukianza na golini kipa Deo Munishi ‘Dida’ amejihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza lakini wenzake, Juma Kaseja na Ally Mustapha ‘Barthez’ ni changamoto kwake na lolote linaweza kutokea kwavile Marcio Maximo hatabiriki.
Juma Abdul ndiye anayetegemewa kucheza beki ya kulia, lakini Salum Telela aliyehamishiwa nafasi hiyo kutoka kwenye kiungo, ni changamoto kwake, ubora wake unaweza kumfanya Maximo abadilishe mawazo kutokana na aina ya mchezo.
Beki ya kushoto anakocheza Oscar Joshua haina upinzani kwani chipukizi, Edward Manyama na Amos Abel wameambiwa mtoto hatumwi sokoni, hivyo wakaushe kidogo.
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani wana uhakika wa kucheza beki ya kati kwani Rajabu Zahir na Pato Ngonyani hawajamshawishi Maximo. Katika kiungo yupo Mbuyu Twite ambaye anafanya vizuri n amewafunika Omega Seme na Said Juma ‘Makapu’. Winga ya kulia Haruna Niyonzima amejihakikishia namba huku Andrey Coutinho akicheza kushoto. Itategemea na mambo kwani Niyonzima anaweza pia kuchezeshwa namba nane halafu Mrisho Ngassa akacheza kulia.
Lakini kwa mfumo wa sasa, Hassan Dilunga ndiye anayecheza namba nane huku Hamis Kiiza akicheza namba 10 akigombea na Ngassa na Simon Msuva ambao hata hivyo watakuwa wanatokea pembeni. Katika namba nane pia wapo Nizar Khalfan na Hamis Thabit.
Kwenye umaliziaji Maximo atamsimamisha Genilson Santos ‘Jaja’ kwavile amejiridhisha na kumpa kazi ya kutupia tu hataki apige vyenga wala nini. Lakini mchezo ukimkataa Jerry Tegete au Hussein Javu watakula shavu.Wengi waliofuatilia mazoezi ya Maximo watabiri kwamba huenda Said Bahanuzi akapewa nafasi kidogo na akafanya mambo ambayo yatampa namba japo kwa dakika 60 kwenye timu na kushangaza wengi.
VIKOSI
Simba
1. Ivo Mapunda, 2. Nassoro Masoud ‘Chollo’, 3. Issah Rashid ‘Baba Ubaya’, 4. Joram Mgeveke, 5. Joseph Owino, 6. Pierre Kwizera, 7. Amri Kiemba, 8. Shaaban Kisiga, 9. Amissi Tambwe, 10. Paul Kiongera, 11. Emmanuel Okwi
Yanga
1 Deo Maunishi ‘Dida’, 2 Juma Abdul, 3 Oscar Joshua, 4 Nadir Haroub ‘Cannavaro’, 5 Kelvin Yondani , 6 Mbuyu Twite, 7 Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, 8 Hassan Dilunga, 9 Geilson Santos ‘Jaja’, 10 Mrisho Ngassa, 11 Andrey Coutinho.
MAKOCHA
Phiri
Phiri anasema; “Nimekaa na hii timu kwa muda mfupi lakini wachezaji wangu wamebadilika na sasa nimepata kikosi ambacho naweza kusema ni cha kwanza, nina kazi ya kujenga safu ya ulinzi baada ya kuondoka Mosoti lakini nitafurahi kama Okwi akiruhusiwa kucheza Simba.”
Maximo
Kocha Maximo sera yake kubwa anataka kufanya kazi kitimu na siyo kikosi chenye wachezaji wachache.; “Napenda kufanya kazi na kundi la wachezaji na siyo mchezaji mmoja, juu ya ‘first 11’ inapatikana kulingana na mechi tunayocheza na namna gani wapinzani wetu watakuja, nataka kucheza mpira wa kasi, basi nitawatumia wachezaji wenye kasi ninayoitaka, nitaka tucheze mpira wa kutulia, nitaanza na wachezaji wenye sifa hiyo, ndiyo maana nasema, nataka kufanya kazi na kundi la wachezaji,” anasema Maximo.
WACHEZAJI
Straika Amissi Tambwe wa Simba anasema kikosi chao cha sasa ni kizuri kulinganisha na kile cha msimu uliopita: “Sasa tupo vizuri hata nisipokuwepo mimi najua Maguli atafanya kazi nzuri, na siyo huyo tu kuna wachezaji wengi wazuri wapo kama Kiongera, Okwi na Kisiga.”
Kipa Ivo Mapunda naye anasisitiza jambo moja tu katika kikosi chao kuwa kipo imara ila bado safu ya ulinzi haijakaa sawa: “Natakiwa kuwa makini kwani safu inayonilinda siyo imara ukilinganisha na alivyokuwepo Mosoti, Mgeveke ni mzuri ila hana uzoefu.”
Kiungo Mbuyu Twite anasema: “Timu iko vizuri sana kwa sasa na ushindani umekuwa mkubwa kwa namna hii mchezaji yeyote akilega, mwingine atachukua nafasi.”
Beki Juma Abdul anasema: “Ushindani uliopo kikosini ni mkubwa, ipo kazi kweli kweli. Kama unavyoona kila nafasi ina mchezaji mzuri zaidi ya mmoja na kufanya ushindani kuwa mkubwa.”