Simba yampandia dau beki wa mpira

Muktasari:

  • Katika dirisha dogo lililopita, Lawi alihusishwa na Simba kwenda kusaidiana na beki Henock Inonga na Che Malone Fondoh, huku Keneddy Juma akitajwa kuachwa, lakini mambo yakaenda sivyo na kusalia Coastal, ambapo Kennedy alibaki Msimbazi, lakini mambo yameanza upya kwa sasa.

UKISIKIA haishi hadi iishe ndio hii. Baada ya kumkosa katika dirisha dogo la usajili la msimu huu, mabosi wa Simba wameamua kumkomalia beki wa kati wa Coastal Union, Lameck Lawi anayetajwa pia kuwindwa na Ihefu kwa kumpandia dau ili kumnasa katika dirisha lijalo.

Katika dirisha dogo lililopita, Lawi alihusishwa na Simba kwenda kusaidiana na beki Henock Inonga na Che Malone Fondoh, huku Keneddy Juma akitajwa kuachwa, lakini mambo yakaenda sivyo na kusalia Coastal, ambapo Kennedy alibaki Msimbazi, lakini mambo yameanza upya kwa sasa.

Mwanaspoti imezinasa habari za ndani kutoka Coastal kuwa Ihefu na Simba zinachuana kuwania saini ya Lawi.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya timu zote mbili vimeliambia Mwanaspoti kuwa, Ihefu imeweka mezani Sh230 milioni kunasa saini ya beki huyo wa kutumainiwa ili kumng’oa kwa Wagosi wa Kaya.

Ili kuipiku Ihefu, taarifa zinasema Simba imepanda dau kwa kuweka Sh250 milioni ili iweze kukamilisha dili la beki huyo ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Wagosi wa Kaya.

“Ihefu ndio walianza kutuma ofa lakini Simba nao wameingia kwa kuonyesha kumuhitaji mchezaji wetu hivyo tuna ofa mbili mezani,” kimesema chanzo hicho.

“Imetumwa ofa ya 230 milioni kwa ajili ya kumpata beki huyo ambaye ni pendekezo la kocha kutokana na mabeki wetu wa kati kupishana mara kwa mara kutokana na kuwa majeruhi, hivyo kocha amesema kuna umuhimu wa kuongeza nguvu eneo hilo.”

Mmoja wa viongozi kutoka ndani ya Ihefu: “Tumemfuatilia kwa ukaribu mchezaji huyo na kuridhishwa na uwezo wake anaweza kuwa msaada mkubwa kikosini kwetu msimu ujao endapo ofa yetu itapokewa na kwenda kama tunavyotarajia.”

Chanzo hicho kimesema mazungumzo kati ya timu hizo mbili yanakwenda vizuri na mambo yakiwa tayari wataweka wazi, lakini sasa wanaendelea kupambana ni namna gani wanaweza kufanikisha hilo.

Mwanaspoti lilipomtafuta beki huyo alikiri bado ni mali ya Coastal Union kwa sababu ana mkataba hadi 2024.

“Sijajua lolote kuhusiana na ofa zilizopo kwani mimi bado ni mchezaji wa Coastal kwa mkataba wa mwaka mmoja, hivyo siruhusiwi kufuatwa na timu yoyote. Wanaonihitaji wanatakiwa kufanya mazungumzo na klabu,” alisema Lawi aliyekichezea pia kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars hivi karibuni na kuongeza kuwa:

“Hakuna timu imenipigia simu wala kunifuata kwa ajili ya mazungumzo yoyote kuhusiana na kuhitaji huduma yangu. Kama hayo unayosema yana ukweli viongozi watanishirikisha mambo yakiwa tayari yamekamilika.”