Prime
Simba yamganda kiungo Sfaxien

Muktasari:
- Simba ilimuona kiungo huyo katika mechi ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ilipoichapa CS Sfaxien Kwa Mkapa kwa mabao 2-1 kisha kwenda kuifunga kwake 1-0.
MABOSI wa Simba wamemganda kiungo wa CS Sfaxien ya Tunisia, Balla Moussa Conte baada ya kufanya naye mazungumzo na sasa wanasikilizia uamuzi wa mwisho wa klabu anayoichezea ili atue Msimbazi msimu ujao.
Simba ilimuona kiungo huyo katika mechi ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ilipoichapa CS Sfaxien Kwa Mkapa kwa mabao 2-1 kisha kwenda kuifunga kwake 1-0.
Hata hivyo Mwanaspoti linafahamu dili hilo liliishia njiani katika dirisha dogo licha ya mazungumzo ya mwisho mchezaji huyo kuwaambia wampe pesa ili asitishe mkataba alionao kwa Waarabu hao.
Taarifa za ndani zinasema Simba ilikubaliana na Conte mwishoni mwa msimu kwamba itampatia pesa ambazo wamekubaliana ili auze mkataba wake na hivi karibuni ilirudi kukumbushia.
“Ili kiungo huyo atue ndani ya Simba inabidi amalize mkataba au auvunje, jambo ambalo hawezi kulifanya kama hatapewa pesa na Wekundu hao,” taarifa zilidai.
Awali, Mwanaspoti liliwahi kuandika kuwa, mara ya kwanza kocha Fadlu Davids alivutiwa na uwezo wa kiungo huyo katika mchezo uliopigwa jijini Dar es Salaam, Desemba 15, 2024 ambapo Simba ilishinda mabao 2-1, huku Conte akicheza dakika zote tisini.
“Baada ya mchezo wa kwanza Fadlu akataka kujidhihirisha mchezo wa pili ambapo pia kiungo huyo alicheza dakika zote tisini kwa kiwango kizuri sana,” kilisema chanzo
Chanzo hicho kiliongeza kuwa baada ya mchezo wa pili uliochezwa Tunisia, Fadlu alimpa jukumu kipa Moussa Camara kuzungumza na Conte ambaye anatoka naye nchi moja ya Guinea.
CONTE NI NANI?
Ni kiungo mkabaji mzaliwa wa Kamsar, Guinea akiwa na uwezo pia wa kucheza nafasi ya kiungo cha ushambuliaji. Kiungo huyo aliyezaliwa Aprili 15, 2004 amekuwa mhimili mkubwa ndani ya CS Sfaixien aliyojiunga nayo Februari Mosi, 2023, huku malezi yake ya soka akiyapata katika Kituo cha Academie La Louvia, Guinea.
Katika kikosi cha CS Sfaxien chenye mchanganyiko wa wachezaji wa mataifa mbalimbali ikiwemo Mali, Algeria, Tunisia, Guinea na Ivory Coast, kiungo huyo ni nyota wa tano kati ya wenye thamani kubwa klabuni.
Katika orodha ya wachezaji wa CS Sfaxien wenye thamani kubwa Mohamed Nasraoui (Sh1.8 bilioni) sawa na Hichem Baccar na Mohamed Dhaoui, ilhali anayefuatia ni Aymen Dahmen (Sh1.7 bilioni), kisha Conte.
Licha ya kwamba Simba ina viungo wakabaji watatu wa kimataifa ambao ni Fabrice Ngoma, Debora Mavambo na Augustine Okejepha, mbali na wazawa Yusuf Kagoma na Mzamiru Yassin, lakiniFadlu anamtaka Conte ili kuongeza ushindani na yupo atakayeng’olewa.
Kati ya nyota hao, Ngoma ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika Juni 30, 2025, anaonekana kuwaka kiasi cha kuhatarisha nafasi za wenzake waliojiunga mwanzoni mwa msimu huu, huku akiandaliwa mkataba mpya.
Kama Simba itamchukua kiungo huyo itabidi mchezaji mmoja wa kigeni atolewe kwenye hesabu za kikosi hicho ili nafasi ipatikane.
Conte mwenye umri wa miaka 20 anatakiwa na Fadlu katika kufanikisha mradi wake wa muda mrefu kuijenga timu hiyo, kwani tangu atue Julai 2024, asilimia kubwa ya wachezaji aliowasajili ni chini ya miaka 25.