Simba yakomaa na Mkenya
MWANASPOTI linajua kwamba Kocha Mkenya, Abdul Idd Salim ana uwezekano mkubwa wa kutua Simba ingawa wanafanya siri kubwa. Kocha huyo ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuwanoa magolikipa Aishi Manula, Benno Kakolanya na Ally Salim.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alieleza miongoni mwa mambo ambayo alikwenda kuyafanya Afrika Kusini ni kuzungumza na mmoja wa makocha wa makipa ambao wanatoka katika nchi hiyo lakini inaonekana dili hilo limekwama.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba bado Simba inakoma na Mkenya huyo ingawa anadengua kwenye dau.
Mwanaspoti lilimtafuta Salim ambaye alielezea kwa ufupi kuwa mawasiliano kati yake na viongozi wa Simba yamefanyika si chini ya mara moja juu ya suala la kumtaka lakini bado hayajafikia mwisho.
Salim wakati yupo Simba aliwanoa makipa, Mghana Daniel Agyei, Peter Manyika Junior ambaye sasa yupo Polisi Tanzania na Denis Richard ambaye anacheza KMC.
Manyika alisema Salim ni moja ya makocha wa makipa wazuri ambao wanaijua kazi.