Simba yajiandaa kwa penalti

Morogoro. Simba SC imehitimisha kambi ya siku nne ya kujiandaa na mchezo nusu fainali Kombe la FA dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Katika mazoezi ya mwisho, jopo la benchi la ufundi chini ya kocha mkuu Joseph Omog ilikuwa na kazi moja ya kusimamia mazoezi ya aina tatu ili kuhakikisha Simba inapata ushindi ndani ya dakika 90 ama kwa njia ya penalti endapo itafikia hatua hiyo na kusonga mbele.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Jackson Mayanja alisema kikosi chao kimefanya mazoezi tofautitofauti kutokana na aina ya mchezo uliopo mbele yao wa nusu fainali ambapo wameanza mazoezi ya viungo, lakini upigaji wa penalti na mashuti ndani na nje ya 18.
“Mchezo uliopo mbele yetu ni mgumu na tumefanya maandalizi ya kutosha ili kujiweka fiti na kukabiliana na kila aina ya upinzani, lakini lengo letu ni kupata matokeo ili tusonge mbele na kucheza fainali ya kombe la FC na kutwaa kombe hilo,”alisema Mayanja.
Mayanja alisema kuwa wamefanyia kazi upigaji wa mipira ya adhabu ya penalti na adhabu nyingine nje ya 18, lakini upigaji wa mashuti ya umbali mrefu na mashuti mafupi.
Katika mazoezi ya hatua ya upigaji wa mipira ya penalti na mashuti nje ya 18, Omog alikuwa mkali kwa wachezaji waliokuwa wakipiga mipira fyongo ama kudakwa na makipa au kutoka nje ya lango.
Wachezaji waliojikuta wakipiga mipira iliyokosa lengo ni pamoja na Bukungu, Mwinyi Kazimoto, Haji Lufungo, Mohamed Ibrahim, Juma Luizio, Jonas Mkude na meneja wa klabu hiyo Mussa Hassan Mgosi aliyejikuta akikumbana na ukali wa kocha huyo baada ya kukosa mpira wa penalti.