Simba yainyatia Yanga

Wednesday May 11 2022
full pic
By Thomas Ng'itu

MNAHESABU lakini! hii ndio kauli ya mashabiki wa Simba baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar mchezo uliochezwa uwanja wa Mkapa leo usiku.

Ushindi huo umepunguza gepu la pointi 11 walilokuwa nalo dhidi ya vinara Yanga wenye pointi 57 na kubakiza pointi nane Simba wakiwa na pointi 49 na kuendelea kusalia nafasi ya pili.

Mabao mawili ya kipindi cha kwanza yaliyofungwa na Kibu Denis na John Bocco yametosha kuwafanya mashabiki wake watoke kifua mbele uwanjani hapa.

Simba katika kipindi cha pili iliingia kwa kuhitaji bao la tatu lakini mipango yao ya mwisho kwenye umaliziaji ilikuwa changamoto.

Dakika 50 Simba ilitaka kupata bao la tatu baada ya Ousmane Sakho kupiga krosi iliyokutana na Kibu Denis ambaye umakini wake kumuangalia kipa wa Kagera Sugar ulikuwa mdogo baada ya kupiga mpira na kuishia mikononi kwa kipa.

Dakika 53 kiungo Ally Idd wa Kagera alipewa kadi ya njano wakati huo huo timu yake ilifanya mabadiliko ya kutoa Hamis Kizza na Ally Idd na nafasi zao waliingia Mbaraka Yusuph na Erick Mwijage.

Advertisement

Mabadiliko hayo yalikuwa yanaenda kuongeza nguvu kwenye eneo la kiungo na ushambuliaji katia timu ya Kagera Sugar.

Dakika 56 kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin alionyeshewa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Mbaraka Yusuph ambaye alikimbia na mpira kwa spidi akipasua katikati ya wachezaji wa Simba.

Kagera ilionekana kuwa na mipango baada ya kufanya mabadiliko lakini bado umaliziaji ulionekana kuwa changamoto.

Dakika 66 Kagera ilifanya mabadiliko mengine akitoka Hassan Mwatelema na kuingia Meshack Mwita kwtika eneo la ushambuliaji wakati huo huo Simba ilimtoa Kibu Dennis na John Bocco na kuingia Peter Banda na Meddie Kagere.

Dakika 72 Simba ilitaka kupata bao la tatu baada ya kugongeana pasi za haraka na Mzamiru Yassin kupiga shuti kali nje ya boksi lakini kipa Said Kipao aliudaka mpira huo.

Dakika 78 Simba ilifanya mabadiliko ya kumtoa Ousmane Sakho na kuingia Yusuph Mhilu kwenye eneo la winga.

Dakika 86 Kagera ilitaka kupata bao la kufutia machozi baada ya mshambuliaji wake Mbaraka Yusuph kufyatuka shuti lakini moira ulipas juu kidogo ya goli.

Dakika 89 Simba ilifanya mabadiliko mengine ya kutoka Henock Inonga na Pascal Wawa na nafasi zao waliingia Israel Patrick na Kennedy Juma.


Advertisement