Simba yaingilia Kwa Mkapa mlango sio

Muktasari:
- Mechi hiyo ya Dabi ya Kariakoo kati ya timu hizo inayotarajiwa kupigwa kuanzia saa 11:00 jioni, imeshuhudia msafari wa Simba ukiwasili mapema Saa 9:26 alasiri na kuzima uvumi wa kususia kucheza kutokana na ukimya wa muda mrefu.
KIKOSI cha Simba kimekuwa cha kwanza kuwasili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika pambano la timu hiyo dhidi ya watani zao Yanga huku ikitumia mlango usiokuwa rasmi wa kubadilishia nguo (Dressing Room).
Mechi hiyo ya Dabi ya Kariakoo kati ya timu hizo inayotarajiwa kupigwa kuanzia saa 11:00 jioni, imeshuhudia msafari wa Simba ukiwasili mapema Saa 9:26 alasiri na kuzima uvumi wa kususia kucheza kutokana na ukimya wa muda mrefu.
Simba ilikuwa kimya wakati wa mechi hiyo hadi leo mchana ilipotoa taarifa ya kushiriki pambano hilo ambalo awali lilipangwa kufanyika Machi 8, 2025, kabla ya kupangwa tena Juni 15 kisha kupelekwa mbele hadi Juni 25, 2025.
Wakati wa kuwasili Kwa Mkapa, msafara wa Simba ulitumia mlango tofauti na ule ambao umepangwa wa kuingilia kwa timu ngeni uliokuwa kwenye chumba cha kufanyia mikutano 'Press Conference'.
Simba iliyofika uwanjani hapo Saa 9:26 alasiri, baada ya kuwasili walianza kushuka watuza vifaa wa timu hiyo wakifuatiwa na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids, kisha wakafuatiwa wachezaji wakiongozwa na kiungo, Yusuph Kagoma.
Pambano hilo lilishindwa kufanyika Machi 8, kwa kile kilichoelezwa na Simba kususia mechi hiyo kutokana na walioelezwa makomandoo wa Yanga kuwazuia kufanya mazoezi siku moja kabla ya miamba hiyo kukutana.
Hata hivyo, baada ya hapo Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), iliahirisha mechi hiyo kwa ilichoeleza kulikuwa pia na viashiria vya rushwa.
Baada ya hapo, pambano hilo likapangwa kufanyika Juni 15, 2025, ambapo Yanga iligoma kucheza hadi matakwa yao manne yatakapotekelezwa katika mkutano wa Bodi ya Ligi (TPLB) na viongozi wa Yanga walipokutana kwa ajili ya kujadili mechi hiyo ya Juni 15.
Katika matakwa hayo manne, Yanga ilitaka Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi Ya Ligi (TPLB), Almasi Kasongo na Mwenyekiti wake, Steven Mguto na Kamati tendaji ijiuzulu ndipo itakapocheza pambano hilo.
Baada ya hapo, Mguto aliandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ya kijiuzulu huku Kasongo akisimamishwa kazi na Rais, Wallace Karia.
Kitendo cha vigogo hao kusimamishwa huku viongozi wa Yanga na Simba wakiitwa Ikulu ya Dodoma na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ilirahishisha mechi hiyo kuchezwa na ndipo ikatolewa tena Juni 15 na kupangiwa Juni 25.