Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yafunga 'file' la viporo kwa kishindo, yazidi kuibana Yanga

VIPORO Pict
VIPORO Pict

Muktasari:

  • Simba ilikuwa na mechi nyingi mkononi kutokana na kushiriki kwao katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho, hali ambayo iliwafanya kuchelewa kucheza mechi kadhaa za ligi huku mpinzani wao, Yanga, akiendelea na ratiba ya kawaida ya ligi.

'FILE' la mechi za viporo ambalo lilikuwa mezani kwa Kocha Fadlu Davids limefungwa rasmi jana Jumapili kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam  baada ya Simba SC kukamilisha mechi nne kwa mafanikio makubwa kwa kukusanya pointi zote 12. Hii imepunguza tofauti ya pointi kutoka 13 hadi moja dhidi ya vinara wa Ligi Kuu, Yanga SC.

Simba ilikuwa na mechi nyingi mkononi kutokana na kushiriki kwao katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho, hali ambayo iliwafanya kuchelewa kucheza mechi kadhaa za ligi huku mpinzani wao, Yanga, akiendelea na ratiba ya kawaida ya ligi.

Katika mchezo wa jana dhidi ya KMC, Simba ilishinda kwa mabao 2-1. Ushindi huo umeifanya timu hiyo.kufikisha pointi 69 baada ya mechi 26, wakibaki nyuma kwa alama moja tu dhidi ya Yanga ambayo nayo imecheza idadi sawa ya mechi. Ligi sasa inaingia katika raundi nne za mwisho huku ushindani ukiwa mkubwa zaidi.

KMC ilikuwa ya kwanza kufungua pazia la mabao katika dakika ya nane kupitia kwa Rashid Chambo ambaye alifunga kwa shuti kali nje ya boksi, likiwa ni bao ambalo kipa Mussa Camara alishindwa kulizuia. Hilo lilikuwa bao la tatu linaloruhusiwa na Camara katika mechi nne za viporo.

Camara ameruhusu mabao katika mechi tatu kati ya nne  dhidi ya Pamba Jiji (5-1), Mashujaa (2-1) na jana dhidi ya KMC. Mechi pekee aliyotoka bila kuruhusu bao ilikuwa dhidi ya JKT Tanzania. Pamoja na kuruhusu mabao hayo, Simba imeonesha uimara kwa kushinda mechi zote hizo.

Simba walijibu haraka bao hilo kwa kusawazisha dakika nane baadaye kupitia kwa Steven Mukwala, aliyeunganisha kazi nzuri ya Joshua Mutale ambaye alianza kwa mara ya tatu mfululizo kwenye kikosi cha kwanza cha Simba. Mukwala aliisawazishia timu katika dakika ya 16.

Hilo lilikuwa bao la 10 kwa Mukwala msimu huu kwenye ligi, likimweka katika nafasi ya tatu kwenye orodha ya wafungaji bora wa Simba nyuma ya Charles Jean Ahoua mwenye mabao 15 na Leonel Ateba mwenye mabao 12. Ushindani huo unaipa Simba nguvu zaidi kwenye safu ya ushambuliaji.

Licha ya kufunga bao hilo, Mukwala alipoteza nafasi mbili za wazi katika dakika tano za nyongeza kipindi cha kwanza, hali ambayo ingeifanya Simba kuingia mapumziko ikiwa mbele. Hata hivyo, alikuja kufuta makosa hayo mapema kipindi cha pili.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, na katika dakika ya 47, Mukwala aliipatia Simba bao la pili baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa KMC na kufunga kwa ustadi mkubwa. Bao hilo lilithibitisha ubora wake na kujibu mapigo ya mshambuliaji mwenzake Leonel Ateba.

Katika mechi iliyopita dhidi ya Pamba Jiji, Ateba alifunga mabao mawili na kumuweka katika nafasi nzuri ya kuwania kiatu cha dhahabu. Ushindani huo wa heshima kati ya Ateba na Mukwala unaifanya Simba kuwa tishio kwa timu pinzani.

Safu ya ushambuliaji ya Simba kwa sasa ndiyo kali zaidi katika ligi ikiwa na jumla ya mabao 38, hali inayompa matumaini makubwa Kocha Fadlu kuelekea katika mechi nne zilizobakia. 

Mechi zilizobaki kwa Simba ni dhidi ya Singida Black Stars, Yanga SC, Kengold  ambayo tayari imeshuka daraja na Kagera Sugar ambayo inahaha kuikwepa nafasi ya kushuka daraja. Hii inaifanya kila mechi kuwa ya fainali kwa Wekundu wa Msimbazi.

Matarajio makubwa kwa sasa yapo kwenye mchezo wa dabi dhidi ya Yanga, mechi ambayo huenda ikaamua bingwa wa ligi msimu huu. Simba inahitaji ushindi katika mechi hiyo ili kupindua kilele cha msimamo.

Mbali na presha ya ligi, Simba pia wanajiandaa kwa mechi mbili za fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco. Mechi ya kwanza itapigwa Mei 17 ugenini, kabla ya kurudiana Mei 25 jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kocha Fadlu Davids amesema anahitaji kikosi chake kiwe na mwelekeo na nidhamu ya hali ya juu kwa kuwa wiki hizi mbili zijazo ni muhimu zaidi katika historia ya msimu wao. “Kila mchezo ni fainali, na kila dakika ni ya dhahabu,” alisema.

Kwa kufunga file la viporo kwa ushindi wa asilimia 100 ndani ya siku 11, Simba imeonyesha dhamira ya dhati ya kurejesha taji la ligi ambalo lilichukuliwa na Yanga kwa misimu mitatu mfululizo. Vita ya ubingwa sasa imefunguka rasmi.