Simba yaanzia Dodoma, Kagere akiwapa furaha mashabiki

Muktasari:
Ndivyo unaweza kusema, Ushindi wa kwanza wa Simba msimu huu umeanzia mkoani Dodoma baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji.
Dodoma. Ndivyo unaweza kusema, Ushindi wa kwanza wa Simba msimu huu umeanzia mkoani Dodoma baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji.
Bao pekee la ushindi la Simba likifungwa na mshambuliaji Meddie Kagere ambaye alitumia vema nafasi moja aliyoipata tangu aingie kufunga bao hilo lililowapa ushindi muhimu Simba.

Kabla ya hapo Simba ilishindwa kufunga bao kwenye mechi zake tatu zilizopita ikiwemo ya kirafiki dhidi ya TP Mazembe, ya Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao wa jadi Yanga na ile ya klwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United.
Ukame huo wa mabao uliwapa hofu mashabiki wa timu hiyo kwenye harakati zao za kutetea tena taji la Ligi Kuu wanaloshikilia kwa misimu minne mfululizo.
Ushindi huo pia umeamsha mbio za Simba kupata matokeo ya ushindi kwenye mechi zijazo za ligi kuu.
Kocha Seleman Matola baada ya mchezo alisema ushindi huo wameupata kwa ugumu ambao kwao ilikua ni muhimu kushinda.
Matola aliongeza kuwa, wapinzani wao walijiandaa kucheza kama vita jambo ambalo lilipelekea mchezo uwe mgumu na wachezaji wao kuumia.
"Tumeshukuru kupata ushindi kwenye mchezo huu ambao hata hivyo ulikua mgumu wenzetu waliingia kupambana kama vita vile iliyopelekea kuumia kwa wachezaji wetu" alisema Matola.
Kocha Mbwana Makata wa Dodoma Jiji kwake alisema aliwaelekeza wachezaji wake kucheza kwa nidhamu kubwa ya mchezo lakini matokeo yamekua tofauti na walivyotarajia kwa kupoteza mchezo huo muhimu.
"Tulijipanga kupata matokeo kwenye mchezo huu ndo sababu wachezaji wangu walicheza kwa presha ya juu lakini bahati haikuwa yetu leo" alisema Makata