Simba wazidi kuinyatia Yanga kileleni

Mchezo wa Ligi Kuu kati ya Kagera Sugar na Simba umemalizika kwenye uwanja wa Kaitaba kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Iliwachukua Simba dakika 12 kupata bao la kwanza kupitia kwa Luis Miquissone aliyepokea pasi safi kutoka kwa Clatous Chama na kuzamisha mpira ndani ya nyavu za Kagera.

Baada ya bao hilo Kagera waliamka kutoka usingizini na kuanza kulishambulia lango la Simba huku weakimiliki mpira kwa dakika zisizopungua tano.

Simba baada ya kuona hivyo walianza kutafuta bao la pili na kwa kasi na dakika ya 23 walipata bao kupitia kwa Chriss Mugalu aliyefunga baada ya kupokea pasi mpenyezo kutoka kwa Hassan Dilunga.

Bao hilo lilidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika na kipindi cha pili kilirejea kwa Kagera kutafuta bao huku mabadiliko yakifanyika kwa timu zote mbili.

Kagera waliwatoa Abdallah Mfuko, Peter Mwalyanzi na Mwaita Gereza huku Dickson Mhilu, Saadat Nanguo,  na Hassan Mwatarema wakiingia.

Kwa upande wa Simba walitoka Mzamiru Yassin, Chriss Mugalu na Hassan Dilunga na nafasi zao kuchukuliwa na Meddie Kagere, Erasto Nyoni na Rally Bwalya wachezaji nwalioingia kulinda mabao mawili ya Simba.

Mpaka dakika 90 zinamalizika Kagera 0-2 Simba. Matokeo hayo yanawafanya Simba kufikisha alama 55 baada ya mechi 23, na kupunguza alama dhidi ya mahasimu wake Yanga waliopo kileleni na alama 57 baada ya mechi 26.

Huko Moshi mechi nyingine ilichezwa ambapo Polisi Tanzania imekubali kichapo vha bao 1-0 kutoka kwa Mbeya City bado likifungwa na Kibu Denis dakika ya 52 ambalo limewasogeza kutoka nafasi ya 17 hadi ya 16 wakifikisha alama 24.

Ruvu Shooting nao wamempapasa Mwadui kwa mabao 5-1 na sasa wamefikisha alama 37 nafasi ya sita.