Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba walaaa, ilishajipanga mapema!

SIMBA ina ratiba ngumu na ya mtego ndani ya mwezi huu ikilazimika kucheza mechi sita ndani ya siku 22 na kati ya hizo, nne itakuwa ugenini, lakini benchi lao la ufundi limesema halina noma kwani wameshajipanga mapema kwa ajili ya kukabiliana nayo na malengo yao ni kuvuna pointi 18.

Kuanzia Jumatano ijayo ya Novemba 9, itakapoifuata Singida Big Stars katika Uwanja wa Liti, mjini Singida, Simba itafuatiwa na mechi za bandika bandua ikiwamo dhidi ya Ihefu itakayopigwa Nov 12, kisha Nov 16 kuvaana na Namungo.

Novemba 19 itakabiliana na Ruvu Shooting ugenini na baada ya hapo Novemba 23 itaifuata Mbeya City na Nov 27 itacheza dhidi ya Polisi Tanzania ugenini katika Uwanja wa Ushirika Moshi.

Kwa wastani, Simba itakuwa na siku tatu za mapumziko na kujiandaa kutoka mchezo mmoja hadi mwingine lakini muda huo unaweza kupungua kutokana na muda wa safari wa kutoka kituo kimoja hadi kingine kwa ajili ya kila mchezo unaofuata hasa zile za nje ya Dar es Salaam.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu aliliambia gazeti hili wamejipanga kukabiliana na ratiba iliyo mbele yao na hawako tayari iwe kisingizio kwao.

“Ratiba ni ngumu kweli lakini mwishowe hatuko peke yetu wenye hiyo ratiba, hivyo hatupaswi kuanza kuilalamikia. Tunatakiwa twende tukakabiliane nayo maana sio sisi peke yetu hata wengine pia nao inawabana.”

“Unacheza tarehe 9 kwa mfano, unalazimika kuondoka tarehe 10 kwa vile miundombinu hairuhusu kusafiri usiku na unaweza kujikuta unatakiwa usafiri kwa basi hadi Dodoma kutoka Singida na unafika Dar es Salaam unabakia na siku moja ya kujiandaa huku bado sijafanya ‘recovery’. Changamoto ipo kiukweli, ligi ngumu na muda hautoshi lakini hatuna namna, inabidi upambane kwa kweli ili ufanye vizuri,” alisema Rweyemamu.

Kocha wa Simba, Juma Mgunda alisema wamejiandaa na ratiba ngumu iliyopo mbele yao.

“Sisi kama timu tunalazimika kuheshimu na kufuata kile kinachopangwa na mamlaka inayosimamia ligi, hivyo kwa vile ratiba tayari ipo, tutajipanga kuhakikisha tunakabiliana nayo na kuona ni kwa jinsi gani tutapata matokeo mazuri,” alisema Mgunda.

Ugumu wa ratiba ambao Simba watakabiliana nao mwezi huu, ni kama ule ambao walikutana nao mwezi uliopita na walicheza mechi sita za mashindano tofauti ndani ya siku 29 ambazo waliangusha jumla ya pointi nne kwa kupoteza mmoja kati ya hiyo na kutoka sare moja.

Ilikuwa na mechi mbili za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Primeiro de Agosto ya Angola ambazo ilishinda zote na kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo, pia ikawa na mechi nne za Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Dodoma Jiji, Yanga, Azam na Mtibwa Sugar na ilishinda mbili, kupoteza moja na kutoka sare katika mechi moja.

Katika hatua nyingine, nyota wawili wa Simba waliokuwa majeruhi, Israel Mwenda na Jimmyson Mwanuke wameungana na kikosi cha timu hiyo baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yanawakabili.

“Kikosi kipo salama na hakuna majeruhi yeyote kwa sasa. Israel Mwenda alishaungana na wenzake kama ilivyo kwa Jimmyson Mwanuke ambaye tayari ameanza kufanya mazoezi na timu ingawa bado hajawa fiti na tayari kwa mchezo unaofuata dhidi ya Singida Big Stars,” alisema Rweyemamu.