Simba wacheze tu Kariakoo Dabi

Muktasari:
- Nimeona kundi fulani la mashabiki wanaojulikana ni wa Simba wanasema hawako tayari kucheza mechi hiyo ambayo imepangwa kuchezwa Juni 25 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
HAPA kijiweni tuna imani Simba itacheza mechi yake ya marudiano ya Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya mtani wake, Yanga ambayo imezoeleka kwa jina la Kariakoo Dabi.
Nimeona kundi fulani la mashabiki wanaojulikana ni wa Simba wanasema hawako tayari kucheza mechi hiyo ambayo imepangwa kuchezwa Juni 25 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Nadhani wanatania tu na mwishowe, timu yao itashuka uwanjani kuikabili Yanga na kufunga msimu wa Ligi Kuu Bara 2024/2025 katika mchezo huo ambao utakuwa ni kama fainali.
Kijiwe kina sababu mbili zinazokifanya iishawishi Simba icheze Kariakoo Dabi katika tarehe mpya ambayo imetangazwa hivi karibuni na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) baada ya mchezo huo kuahirishwa mara mbili tofauti.
Sababu ya kwanza ni kuheshimu tu mamlaka kama ambavyo Simba ilikuwa inatamba katika kipindi kile ambacho wenzao Yanga walipotangaza kugoma na Simba ilikuwa inasema yenyewe inaheshimu mamlaka za juu, hivyo itacheza.
Sasa haiwezekani siku chache zilizopita walewale waliokuwa wanatusisitiza wanaheshimu na kutii mamlaka, leo hii tena wamegeuka na baadhi wanahamasishana kwenda kinyume na kilichoamriwa na mamlaka zilezile.
Kuna sababu ya pili ambayo ni utayari ambao wao Simba walikuwa wanatuambia wanao kukabiliana na watani wao na huku mtaani wakawa wanatuambia ligi msimu huu haiwezi kumalizika bila Yanga kukutana na Elie Mpanzu Kibisawala.
Ukishakuwa tayari unatakiwa uingie uwanjani ucheze na uhakikishe unapata matokeo mazuri ili kuthibitisha kwa wale uliowaambia unaitaka mechi na watani wasikukimbie.
Kama timu nzuri wanayo hakuna sababu kuiga kile kilichokuwa kikifanywa na watani wao hapo nyuma cha kutishia kugomea mechi.