Sopu ameanza kujipata Azam FC

Muktasari:
- Kauli ya Taoussi inajiri baada ya nyota huyo kuchangia mabao mawili juzi katika ushindi wa timu hiyo wa 5-0, dhidi ya Tabora United, ambapo Sopu alifunga moja na kuasisti pia moja na kufikisha mabao mawili msimu huu na asisti zake nne.
KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Abdul Suleiman ‘Sopu’ ameanza kujipata ndani ya kikosi hicho baada ya kutokuwa na msimu mzuri, jambo linalompa matumaini kocha wa timu hiyo, Rachid Taoussi akitarajia makubwa kutoka kwa nyota huyo.
Kauli ya Taoussi inajiri baada ya nyota huyo kuchangia mabao mawili juzi katika ushindi wa timu hiyo wa 5-0, dhidi ya Tabora United, ambapo Sopu alifunga moja na kuasisti pia moja na kufikisha mabao mawili msimu huu na asisti zake nne.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Sopu alifunga katika dakika ya 11 na mengine yakifungwa na Gibril Sillah aliyetupia mawili dakika ya 16 na 30, huku Idd Seleman ‘Nado’ akifunga pia dakika ya 45 na Nassor Saadun dakika ya 89.
Akizungumza na Mwanaspoti, Taoussi alisema nyota huyo amerejea katika ubora, hivyo mashabiki watarajie mambo mazuri hususani kuanzia msimu ujao, kutokana na kipaji kikubwa alichonacho, ambacho ni hazina ya kufikia malengo ya timu hiyo.
“Napenda kila mmoja wao anavyotimiza majukumu yake, huwezi ukafanya jambo kwa ubora uleule siku zote, ni lazima ukubali kuna siku tu utakuwa chini ya kiwango, nafurahia kuona akirejesha hali yake ya kujiamini kwani inampa motisha,” alisema Taoussi.
Tangu nyota huyo ajiunge na Azam, Julai 4, 2022, akitokea Coastal Union, amekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka katika kikosi hicho, ingawa taratibu anaanza kuonyesha ni kwa nini matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam walihitaji saini yake.
Msimu wa kwanza wa 2022-2023 akiwa na Azam, Sopu alifunga mabao sita ya Ligi Kuu ukiwa ndio bora zaidi kwake tangu ajiunge na kikosi hicho, kwani msimu uliopita wa 2023-2024, kiungo huyo mshambuliaji alifunga bao moja tu.
Msimu huu ambao ni wa tatu kwake kukichezea kikosi hicho, tayari amechangia mabao sita ya Ligi Kuu Bara, akifunga mawili na kuasisti manne, ingawa msimu bora ulikuwa wa 2021-2022, akiwa Coastal Union, alipomaliza msimu na mabao saba.
Mbali na hilo, msimu huo wa 2021-2022, nyota huyo aliibuka mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho la (FA) baada ya kufunga mabao tisa, akiiwezesha Coastal kufika fainali japo ilipoteza mbele ya Yanga kwa penalti 4-1 baada ya dakika 120 timu hizo kufungana 3-3 yeye akipiga hat trick.