Simba v Mashujaa dakika 90 zenye majibu matatu

Muktasari:
- Ijumaa ya leo, timu hizo zinakutana tena katika msako mwingine wa pointi tatu ndani ya Ligi Kuu Bara katika mechi itakayokuwa ikijibu maswali matatu muhimu.
ZIMEPITA takribani siku 182 tangu mara ya mwisho Steven Mukwala afunge bao kwa kichwa katika dakika ya 90+7 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma wakati Simba ikiichapa Mashujaa 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara. Hiyo ilikuwa Ijumaa ya Novemba Mosi, 2024.
Ijumaa ya leo, timu hizo zinakutana tena katika msako mwingine wa pointi tatu ndani ya Ligi Kuu Bara katika mechi itakayokuwa ikijibu maswali matatu muhimu.
Simba inaikaribisha Mashujaa kwenye Uwanja wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam, ikiwa zimeshapita siku 48 tangu ilipocheza mara ya mwisho katika Ligi Kuu ilipoikandika Dodoma Jiji kwa mabao 6-0 siku ya Machi 14. Mechi ya leo ni kiporo cha ligi hiyo, huku wenyeji wakiingia uwanjani wakiwa na mzuka wa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika siku chache zilizopita.
Ni mechi inayotoa majibu matatu tu. Jibu la kwanza, Mashujaa itafuta uteja mbele ya Mnyama wa mechi tatu mfululizo? Pili, Mashujaa itaponea mtego wa play-off, lakini la tatu, Simba itashinda ili ibakize mechi moja kufuzu rasmi Ligi ya Mabingwa msimu ujao? Majibu yatapatikana KMC.
Katika mchezo huu, Mashujaa ina kazi kubwa ya kufanya kuipenya ngome imara ya ulinzi iliyonayo Simba kwani hadi sasa ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache zaidi kwenye Ligi Kuu msimu huu ambayo ni manane.
Mashujaa iliyofunga mabao 26 katika mechi 26, ina wastani wa kufunga bao moja kwa mechi, hivyo nyota wa timu hiyo wakiongozwa na David Ulomi ambaye ni kinara wa mabao kikosini hapo akifunga matano, Seif Karihe na Jafar Kibaya wenye matatu kila mmoja, jukumu lipo kwao kutikisa nyavu za Simba zinazolindwa na kipa Moussa Camara na mabeki wake, Chamou Karaboue, Abdulrazack Hamza, Mohamed Hussein na Shomari Kapombe.
Ikiwa nafasi ya kumi kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi 30 sawa na KMC, Mashujaa inafahamu kwamba inahitaji kushinda mechi tatu kati ya nne zilizobaki ili kuwa salama kabisa kuepuka kushuka daraja kwani ikiteleza kidogo tu, inaweza kuangukia kwenye eneo la kucheza mechi za mchujo (play off) kuwania kubaki Ligi Kuu. Viongozi wao wamedai kwamba wanaanza kusaka upenyo wa kuachana na playoff kuanzia Dar.
Wakati hesabu za Mashujaa zikiwa hivyo, Simba inaanza harakati zake za kuifukuza Yanga kileleni kwani ina viporo vinne hadi kufikia michezo 26 itakayokuwa sawa na watani wao.
Kwa sasa Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 70, imeiacha Simba pointi 13, hivyo ushindi dhidi ya Mashujaa utapunguza gepu hilo na kubaki 10.
Kwenye ligi, Mashujaa haina rekodi nzuri mbele ya Simba kutokana na kupoteza mechi zote tatu walizokutana huku wakiwa hawajafunga bao lolote.
Rekodi zinaonyesha Mashujaa ambayo huu ni msimu wa pili kushiriki Ligi Kuu Bara, dhidi ya Simba ilianza kupoteza 1-0, kisha 2-0 na baadaye 1-0.
Simba ina rekodi nzuri ikiwa uwanja wa nyumbani kufuatia kucheza mechi 11 na kupoteza moja tu, huku ikishinda nane na sare mbili. Imefunga mabao 30 na kuruhusu matano.
Kwa jumla, Simba imecheza mechi 22 ikishinda 18, sare tatu na kupoteza moja ikifunga mabao 52 na kuruhusu manane ikikusanya pointi 57.
Mashujaa inapokuwa uwanja wa ugenini, rekodi zinaonesha haina matokeo mazuri kwani imeshinda mechi moja tu dhidi ya Coastal Union kati ya 13 ilizocheza, sare zikiwa tano na vichapo saba.
Timu hiyo wakati inapoteza mchezo wa duru la kwanza dhidi ya Simba, ilikuwa ikifundishwa na Abdallah Mohamed ‘Baresi’ lakini sasa mikoba yake imechukuliwa na Salum Mayanga.
Mayanga ndani ya Mashujaa, tayari ameiongoza timu hiyo katika michezo mitatu ya ligi akishinda miwili ya kwanza dhidi ya Fountain Gate na Tabora United zote kwa ushindi wa 3-0 nyumbani, kisha akafungwa 2-1 na Namungo ugenini.
Kupoteza mchezo wa ugenini dhidi ya Namungo, unatoa picha ya kwamba bado tatizo la Mashujaa kutopata ushindi ugenini ni kazi aliyonayo Mayanga kuhakikisha anaondoa rekodi hiyo mbaya.
Mashujaa mechi tano za mwisho ugenini kwenye ligi imepoteza nne na sare moja wakati Simba mechi tano za mwisho nyumbani imeshinda nne na sare moja.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Simba, Mayanga alisema: “Tunakutana na timu timu bora ambayo ina matokeo mazuri kwenye michuano inayoshiriki, ili kukabiliana nayo tumefanya maandalizi bora.”
“Ni mechi kubwa na ya ushindani kwani tunacheza na timu ambayo inarejea kusaka nafasi ya kutwaa taji ambalo wamelipoteza kwa misimu mitatu na sisi tunapambana kujihakikishia nafasi ya kucheza ligi msimu ujao, hivyo hautakuwa mchezo rahisi.â€
Kwa upande wa Kocha wa Simba, Fadlu Davids, akili yake inawaza mechi hizi za viporo huku pia akifahamu mbele yake kuna mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane.
Katika kuhakikisha mechi hizo zote anapata matokeo mazuri, alisema: “Kila mechi ina umuhimu wake, tumefanya maandalizi ambayo tunaamini tutafanya vizuri, lengo likiwa ni kupata ushindi ingawa tunafahamu tunakutana na mpinzani mgumu.”
Mbali na Simba kusaka ushindi utakaowafanya kuisogelea Yanga, pia nyota wa kikosi hicho Jean Charles Ahoua ana wakati mwingine mzuri wa kurudisha utawala wake wa kufunga mabao baada ya hivi sasa kuzidiwa moja na kinara Clement Mzize wa Yanga.
Kabla ya Simba kuwa na viporo hivyo vinne, Ahoua alikuwa anaongoza kwa mabao akifunga 12 ambayo sasa yamefikiwa na mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube, akipitwa na Mzize lakini chini yake kuna Jonathan Sowah wa Singida Black Stars mwenye 11.