Simba sasa yahamia kwa mrithi wa Chama
Baada ya kuinasa saini ya mshambuliaji Pa Omar Jobe, Simba sasa inahaha kusaka kiungo mshambuliaji wa maana kabla ya dirisha la usajili halijafungwa leo saa 5:59 usiku.
Mezani kwa mabosi wa Simba kuna majina matatu mazito wakiyachakata kabla ya kufanya uamuzi wa yupi asaini mkataba na wekundu hao.
Kocha Abdelhak Benchikha amewataka viongozi wa Simba kumletea kiungo huyo atakayekwenda kuongeza ufanisi kwenye idara ya kiungo ya timu hiyo.
Endapo Simba itampata mtu wa maana, mashabiki wa Simba wajiandae kutomuona tena kiungo wao fundi Clatous Chama ambaye anaweza kuachwa kwenye dirisha hili la usajili.
Mwanaspoti linafahamu hata kama Simba itamkosa mrithi wa Chama sasa kuna uwezekano mkubwa wekundu hao wakaachana na Mwamba wa Lusaka mwisho wa msimu huu utakapomalizika.
Chama anatumikia adhabu ya kusimamishwa na Simba baada ya kudaiwa kukwaruzana na kocha wa viungo wa timu hiyo ingawa wakati huu kiungo huyo fundi yupo nchini Ivory Coast na timu ya Taifa lake ya Zambia 'Chipolopolo' kwenye Fainali za Mataifa Afrika zinazofanyika nchini humo.