Simba piga haooo Asec!

SIMBA inashuka uwanjani usiku wa leo kuvaana na Asec Mimosas ya Ivory katika mechi ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku nyota wa zamani wa timu hiyo, Fikiri Magosso akiwataka wachezaji kupambana kuandika rekodi.
Simba iliwahi kuvaana na Asec 2003 katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi na kuifumua Dar kwa 1-0 kisha kufungwa ugenini 4-3 na Magosso alisema Simba ikikaza Benin inatoboa.
Simba ikishinda mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Generali Mathieu Kerekou mjini Cotonou, Benin itafikisha pointi 9 zitakazoiweka nafasi nzuri ya kutinga robo fainali na kuwa ya kwanza Tanzania kufanya hivyo katika shirikisho tangu ibadilishwe mfumo 2004.
Magosso aliwataka wachezaji wa Simba kutumia vyema dakika 90 za mchezo huo wa marudiano dhidi ya Asec Mimosas kupata matokeo mazuri na kuweka rekodi ya kufuzu robo fainali ikiwa ugenini.
Simba imetinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa mara mbili 2019 na mwaka jana ikiwa ardhi ya nyumbani, lakini ikishinda itakuwa klabu ya kwanza nchini kwani licha ya mara tatu Yanga na Namungo kutinga makundi ya Shirikisho 2016, 2018 na 2021 hazikufuzu robo fainali.
“Mchezo huu kwa yeyote atakayetumia vizuri dakika 90 atapata matokeo maana hao Asec nao wapo ugenini kama Simba. Wachezaji wa Simba wajitume tu na kujua majukumu,” alisema Magoso aliyeongeza kuwa hana hofu na Simba katika mchezo huo.