Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba ndo hivyo buana!

Muktasari:

Simba ikiwa na mzuka wa ushindi wao wa mechi ya kwanza dhidi ya Ihefu, huku ikiwa na majembe yake yote kikosini, waliduwazwa na Mtibwa kwa sare ya 1-1.

MASHABIKI wa Simba walipiga kelele sana, wakati watani wao, Yanga walipoianza Ligi Kuu Bara kwa sare, lakini jana walijikuta wakisonya kwa hasira baada ya Wakata Miwa wa Manungu, Mtibwa Sugar kuwatibulia kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.

Simba ikiwa na mzuka wa ushindi wao wa mechi ya kwanza dhidi ya Ihefu, huku ikiwa na majembe yake yote kikosini, waliduwazwa na Mtibwa kwa sare ya 1-1.

Hii ni sare ya pili kwa Mtibwa baada ya ile ya awali dhidi ya Ruvu Shooting, huku kiungo wao, Mzamiru Yassin akiendeleza moto msimu huu kwa kufunga bao lake la pili.

Mzamiru aliyesajiliwa na Simba misimu mitano iliyopita akitokea Mtibwa alifunga bao la kuongoza sekunde chache kabla ya mapumziko, huku akishangilia kwa kunyanyua mikono juu kama ishara ya kuwaomba radhi mabosi wake wa zamani.

Mzamiru pia alifunga bao la ushindi la Simba dhidi ya Ihefu kwenye mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya na Wekundu wa Msimbazi kushinda mabao 2-1.

Hata hivyo sekunde chache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili Mtibwa ilichomoa bao kupitia straika wao Mganda, Zirintusa Boban baada ya kuizidi maarifa safu ya ulinzi ya Simba.

MCHEZO ULIVYOKUWA

Katika pambano hilo lililohudhuriwa na mashabiki lukuki, timu zote zilishambuliana kwa kasi, huku zikisababisha kosakosa nyingi.

Kocha Sven Vandenbroeck, aliwaanzisha tena kwa pamoja Joash Onyango na Kennedy Juma kama mabeki wa kati, huku akimpa nafasi Luis Miquissone aliyekosa mchezo wa jijini Mbeya na nyota huyo aliongeza uhai kwenye safu ya mbele ya Simba.

Nahodha wa Simba, John Bocco na wenzake watajilaumu kwa kushindwa kutoka na ushindi kutokana na kupoteza nafasi kadhaa walikokuwa wakizipata mbele ya lango la Mtibwa.

Uzoefu wa Haruna Chanongo, Salum Kanoni na Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ ulikuwa na faida wa kukituliza kikosi hicho kucheza kwa utulivu tofauti na dakika tano za mwanzo na kuwapa kashkash mabeki wa Simba waliokuwa chini ya Onyango na Kennedy licha ya kukosa mabao.

Licha ya Bernard Morrison kushirikiana na Clatous Chama, licha ya kuchachafya ngome ya Mtibwa na kuchezwa madhambi mara kadhaa hakuwa na maajabu kabla ya kutolewa kipindi cha pili kumpisha Mfungaji Bora, Meddie Kagere.

Kocha Sven Kocha alimtoa pia Mzamiru na kumwingiza Francis Kahata huku Mtibwa ikimtoa Ahmed na kumwingiza Salum Kihimbwa, mabadiliko ambayo hayakuleta mabadiliko kwani hadi dakioka 90 zikikamilika kila timu ilikuwa imevuna pointi moja na bao moja.

Sare hiyo kwa Simba ilikuwa ya kwanza tangu Julai 23, mwaka huu dhidi ya Coastal Union katika mechi yao ya msimu uliopita, kwani katika mechi zake za mashindano ilizocheza tangu baada ya sare hiyo imeshinda zote.

Iliifunga Yanga 4-1 katika nusu Fainali ya Kombe lam ASFC kisha kuinyoa Namungo mabao 2-1 katika fainali na kushinda tena 2-0 dhidi ya Namungo kwenye Ngao ya Jamii na baasdaye kuisambaratisha Ihefu kwa mabao 2-1 wiki iliyopita.

Kocha wa Simba naye aliendelea kufanya mabadiliko, alimtoa Mzamiru ambaye alifunga bao dakika ya 45, akamuingiza Francis Kahata, kwa upande wa Mtibwa Sugar alitoka Ahmed akaingia Salum Kihimbwa.

Vikosi vilivyoanza;

MTIBWA:

Mshery, Kanoni, Baba Ubaya, Job, Luseke, Majogoro, Chanongo, Nyangi, Hilika, Boban na Jojo

SIMBA:

Manula, Kapombe, Tshabalala, Onyango, Kennedy, Mkude, Morrison, Mzamiru, Bocco, Chama na Luis

KMC WANATAKA NDOO

Katika mechi nyingine ya jana jioni, KMC wameendelea kuonyesha dhamira yao ya kubeba ndoo baada ya kuwatungua maafande wa Tanzania Prisons kwa mabao 2-1, huku mjini Dodoma mechi ya mapema mchana wenyeji Dodoma Jiji waliendeleza kugawa dozi jijini humo.

KMC walirejea kileleni baada ya kuenguliwa kwa muda na Azam walioshinda juzi usiku mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Azam Complex, baada ya mabao ya Hassan Kabunda dakika ya 21 na lile la jioni la Kenneth Masumbuko kuwapa alama tatu nyingine jijini Dar.

Prisons waliotoka sare ya 1-1 na Yanga ilipata bao lake la kufitioa machozi dakika ya 39 likiwekwa kimiani na Kassim Mdoe na matokeo hayo yamezifanya timu za jiji la Mbeya kutopata ushindi mpaka sasa kwenye ligi hiyo iliyopo raundi ya pili.

Kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma mabao ya Jamal Mtegeta dakika 50 na la straika wa zamani wa Alliance na Gor Mahia ya Keny, Dickson Ambundo yaliipa ushindi wa pili mfululizo wageni wa ligi hiyo, Dodoma Jiji baada ya kuifyatua JKT Tanzania katika Dodoma Derby.

Ushindi huo umeifanya Dodoma kula sahani moja ya KMC na Azam kileleni japo wanatofautishwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. KMC wapo kileleni kwa mabao yao sita ya kufunga na kufungwa moja, huku Azam na Dodoma zikilinagana kila kitu ila zikitofautishwa kwa herufi tu, kwani kila moja ina pointi sita na mabao matatu ya kufunga.

Ligi hiyo itaendelea leo kwa mechi tatu ikiwamo ile ya Yanga dhidi ya Mbeya City ambao ilianza ligi vibaya kwa kucharazwa mabao 4-0 na KMC.

Imeandikwa na Olipa Assa, Oliver Albert, Charles Abel na Jalilu Matereka