Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kapombe aelezea Waarabu watakavyokanyaga moto Amaan Complex

KAPOMBE Pict

Muktasari:

  • Wamepigwa mishale mingi lakini bado wapo imara ndani ya kikosi cha kwanza wakimpambania Mnyama

SIMBA ina mafaza wawili tu kwasasa na wote wapo kikosi cha kwanza. Shomari Kapombe na Mohammed Tshabalala.

Wamepigwa mishale mingi lakini bado wapo imara ndani ya kikosi cha kwanza wakimpambania Mnyama.

Msimu huu hatimae wamecheza fainali yao ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo inahitimishwa Jumapili kwa dakika 90 zitakazoamua nani abebe Kombe. Simba inalazimika kushinda mabao 3-0 ili kuweka heshima yao mpya Afrika.

Kapombe ambaye yupo Simba kwa vipindi tofauti tangu mwaka 2011, ameliambia Mwanaspoti kwamba Berkane watapitishwa kwenye tanuru la moto ndani ya Uwanja wa Amaan kwani Mnyama hatakubali fedheha mbele ya mashabiki wake.

"Tutawapa wakati mgumu waone uwanja kama kaa la moto tofauti na inavyochukuliwa kuwa, tunakuwa hatari tu Kwa Mkapa,"alisema Kapombe na kuongeza kuwa mechi hiyo si ya kawaida. Ni fainali iliyobeba heshima kwa Tanzania. Na sasa wamepania kuandika historia kwa kuifuta aibu ya kupoteza mabao 2-0 katika mechi ya kwanza Morocco.

“Tuna mzigo mkubwa, tunatakiwa kusawazisha mabao mawili haraka na kisha kutafuta ushindi. Lakini tuna silaha kubwa tupo nyumbani. Mashabiki wetu ni nguzo kuu ya ushindi wetu,”alisema Kapombe ambaye ni staa wa zamani wa Ashanti ya Ilala.

Beki huyo wa kulia alisema kama Berkane iliweza kujaza uwanja wao, basi Watanzania nao wanapaswa kujitokeza kwa wingi kuujaza Amaan na kuibadilisha kuwa kama kaa la moto kwa wageni.

"Tunataka hali ile ile kama waliyoifanya kwao,” alisema Kapombe ambapo katika mechi ya kwanza, Simba ilikumbana na dhoruba mapema baada ya Mamadou Camara kufunga bao la kwanza dakika ya nane, kabla ya Oussama Lamlaoui kuiongezea Berkane bao la pili dakika ya 14. Mabao hayo yaliiumiza Simba, lakini yamezidi kuwajaza hasira.

Kapombe alisisitiza kuwa hawatakubali kurudia makosa yale yale. “Tulijifunza, tumerekebisha, na sasa tunarudi na ari mpya. Tunahitaji dakika 90 za umoja, nidhamu, na presha ya mashabiki. Tupo tayari.”

Taarifa kutoka ndani ya kikosi zinaeleza kuwa wachezaji wamewekewa mikakati ya kuanza kwa kasi na kutumia uwanja wa Amaan kama silaha ya kisaikolojia dhidi ya Berkane.

Wachezaji kama Ellie Mpanzu, Kibu Denis, Steven Mukwala na Charles Ahoua wameshawahi kuonesha uwezo mkubwa kwenye mechi kubwa, na safari hii Simba wanahitaji ubora wao kwa kiwango cha juu zaidi.

Berkane kwa upande wao wanajua nini kinawangoja. Wametua Zanzibar wakiwa makini, kulinda uongozi wao wa mabao mawili, lakini pia wakifahamu presha ya kucheza mbele ya mashabiki wa Simba, waliopania kuona historia ikiandikwa kwenye ardhi ya Tanzania.

Nini maoni yako. Tuandikie; 0658-376 417